Thursday, July 26, 2012

Watatu wafa katika ajali tofauti tofauti mkoani Dodoma



Na. Luppy Kung’alo, Jeshi la Polisi Dodoma

Watu watatu wamepoteza maisha katika matukio matatu tofauti ya Ajali za Usalama Barabarani jana na kuacha wengine majeruhi katika Mkoa wa Dodoma.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi Bw. Edmund Urio alisema tukio la kwanza lilihusisha Mpanda PikiPiki kugonga Mkokoteni ambalo lilitokea siku ya Jumatano tarehe 26/07/2012 majira ya saa sita na dakika tano usiku katika Barabara kuu ya Dodoma /Morogoro eneo la Kibaigwa Wilayani Kongwa

Akizungumzia tukio hili Bw. Edmund Urio alisema kwamba Piki Piki No. T. 202 BDH aina ya FERICON iliyokuwa ikiendeshwa na Joseph Hekela mweye umri wa miaka (27) Mkazi wa kibaigwa iligonga Mkokoteni kwa nyuma uliokuwa ukiendeshwa Barabarani na kusababisha kifo kwa Mpanda pikipiki huyo.

Kamanda Edmund Urio alisema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa mwendesha Pikipiki kwa kutofuata sheria kwani hakupaswa kuwa katika mwendo wa kasi, na kwa mujibu taratibu taa zake zinapaswa kumulika umbali wa mita mia tatu hivyo alipaswa kuuona mkokoteni huo uliokuwa mbele yake.

“Muendesha Mkokoteni naye ana makosa kwani muda wa chombo hicho kutumia Barabara mwisho wake ni saa kumi na mbili jioni, sasa mpaka muda huo wa saa sita usiku kuwepo barabarani ni makosa” Alifafanua Kamanda Urio

Bw. Edmund Urio alisema Muendesha Mkokoteni huo  amekimbia na anatafutwa kwa kosa la kuendesha mkokoteni kwa muda usioruhusiwa na pindi atakapo kamatwa atachukuliwa hatua za kisheria kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zinavyotaka.

Katika ajali nyingine iliyohusisha mpanda Pikipiki kuwagonga watembea kwa miguu na kusababisha kifo na majeruhi, Kamanda Edmund Urio Alisema ilitokea mnamo tarehe 25/07/2012 majira ya saa moja na dakika saba jioni (19:07hrs) katika eneo la Ipagara Kata ya Ipagara na Wilaya ya Dodoma kwenye Barabara kuu ya Dodoma/Morogoro.

Akizungumzia ajali hiyo alisema Pikipiki No. T. 662 BKC aina ya LIFAN iliyokuwa ikiendeshwa na mtu asiyefahamika  jina  iliwagonga watembea kwa miguu wawili na kusababisha kifo cha mmoja wao aliyejulikana kwa jina la Theresia Chansi mwenye umri wa miaka (37) mgogo na mkazi wa Ipagara amabaye alifariki wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.

 “Katika Ajali hiyo kulikuwa na majeruhi wawili ambao ni Mpanda Piki Piki mwenyewe ambaye amepoteza fahamu na amelazwa wodi namba (1) pamoja na Magreth Daniel mwenye umri wa miaka (40) na mkazi wa Ilazo mjini Dodoma ambaye naye amelazwa katika hospitali hiyo ya mkoa wodi namba (10).” alieleza Bw. Edmund Urio.

Kaimu Kamanda huyo wa Mkoa wa Dodoma alisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo wa kasi aliokuwa akiendesha mpanda Pikipikki huyo, uliosababisha kushindwa kudhibiti Piki piki yake wakati wakinamama hao walipokuwa wakivuka barabara.

Aidha katika tukio la tatu Kamishna Msaidizi huyo wa Jeshi la Polisi Bw. Edmund Urio alisema gari No. T 668 AYQ aina ya FUSO lilokuwa likiendeshwa na Bw. Philipo Wami mwenye umri wa miaka (30) mkazi wa Msanga liliacha njia na kupinduka kisha kusababisha kifo kwa mtu mmoja aliyetambulika kwa jina la Henry Wami mwenye umri wa miaka (19) na mkazi wa Msanga.

Alisema ajli hiyo lilitokea tarehe 25/07/2012 majira ya saa moja kamilia asubuhi (07:00 hrs) katika maeneo ya Kijiji cha Msanga Wilaya ya Chamwino.

Kamanda Edmund Urio alisema Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa chanzo cha ajali hiyo ni kutokana na kushindwa kufanya kazi kwa mfumo wa usukani, uliosababisha gari hiyo kupoteza muelekeo na kupinduka.

Hata hivyo Kamanda Edmund Urio amewaasa watumiaji wote wa barabara kuwa makini na matumizi sahihi ya bararabara ikiwa pamoja na kufuata na kuheshimu sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika.

No comments:

Post a Comment