Tuesday, November 6, 2012

msaada wenu unahitajika kuokoa hali ya msanii rehema chalamila a.k.a ray c


Mwanamuziki muimbaji Rehema Chalamila maarufu kama RayC amekumbwa na tatizo kubwa la kuathirika na madawa ya kulevya. Kwa sasa yumo katika hatua za matibabu ya kujaribu kuondokana na tatizo hilo. 

Kwa kadri ya maelezo ya mama yake dawa ambazo anahitaji kuzitumia ili kuponi ni gharama na pia kama wote tunavyofahamu pia mgonjwa yoyote anatakiwa kula vizuri, mzigo huu ni mkubwa kwa huyu mama, kwa hiyo kunahitajika msaada wa kubeba mzigo huo. 

Wapenzi wa muziki wa binti huyu na watu wenye mapenzi mema tunaweza kumsaidia mama huyu kwa kumtumia kiasi chochote cha fedha kwa kutumia huduma ya tigo pesa kupitia namba 0655999700 

Natanguliza shukrani kwa wote watakao weza kutoa msaada wowote kwa ajili ya matibabu ya mwenzetu

Habari hii kwa hisani ya Mzee Kitime-Mwanamuziki Mkongwe hapa nchini.

RAIS KIKWETE AMPA POLE KATIBU WA MUFTI WA ZANZIBAR ALIYEMWAGIWA TINDIKALI

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akimjulia hali na kumpa pole Katibu wa Mufti wa Zanzibar Sheikh Fadhili Soraga ambaye amelazwa katika chumba cha dharura katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kufuatia majeraha ya usoni na kifuani yaliyotokana na  kurushiwa Tindikali na watu wasiojulikana wakati akifanya mazoezi katika Kiwanja cha Mwanakwerekwe mjini Unguja juzi. Rais ambaye amerejea  leo Jumanne Novemba 6, 2012 akitokea katika ziara ya kikazi ya  takriban juma moja katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Manyara na Singida, amemtakia Sheikh Soraga nafuu ya haraka.PICHA NA IKULU

KUTOKA VIWANJA VYA BUNGENI MJINI DODOMA JANA

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza na Mbunge wa Kibakwe na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, Bungeni Mjini  Dodoma Oktoba  6, 2012.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akiteta na Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda Magalle kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma, Oktoba 6,2012.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akiongea na Mbunge wa Mpedae, Salim Hassan  Abdullah Turky  kwenye viwanja vya Bunge Mjini Dodoma,Oktoba 6, 2012.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

MAKAMU WA RAIS DKT. BILAL AFUNGUA MKUTANO WA 8 WA KIMATAIFA WA BIMA JIJINI DAR JANA

 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akihutubia wakati akifungua mkutano wa 8 wa Kimataifa wa Bima, ulioanza leo katika ukumbi wa Blue Peal, jijini Dar es Salaam. Mkutano huo unatarajia kumalizika Novemba 8 mwaka huu.
 Baadhi ya washiriki wa Mkutano huo wa Kimataiafa wa Bima, kutoka mataifa mbalimbali wakimsikiliza Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, wakati akihutubia, katika ukumbi wa Blue Peal, leo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akifurahia ngoma ya asili wakati akiwasili kwenye Ukumbi wa Blue Peal, jijini Dar es Salaam, leo kwa ajili ya kufungua mkutano wa 8 wa Kimataifa wa Bima, ulioanza leo Novemba 6, 2012 ukitarajia kumalizika Novemba 8, mwaka huu.

BODABODA JIJINI MBEYA WAVAMIA KITUOCHA KUUZIA MAFUTA KWAAJILI YA KUHAKIKISHIWA KWELI HAKUNA MAFUTA AU YANAFICHWA

 VIJANA WA BODA BODA WAKIWA WAMEVAMIA KITUO CHA ORXY KUTAKA KUJUA  KAMA KWELI KUNA MAFUTA AMA LAH.
 HAPA KILA MTU ANATAKA KUSHUHUDIA KAMA MAFUTA YAPO AMA LAH
 MENEJA WA KITUO HICHO ALIYE VAA SHATI JEUPE AKIJARIBU KUWATULIZA WATEJA AMBAO WANA JAZBA KUBWA YA KUTAKA KUJUA KAMA KUNA MAFUTA AU LAH , NA KUWAMBIA KUWA WANGOJE KWANZA ACHUKUE VIFAA ILI AWAONESHE KUWE KWELI HAKUNA  MAFUTA.
 MKUU WA POLISI WILAYA YA MBEYA NAE ALIKUWEPO ENEO LA TUKIO,KUWATULIZA VIJANA HAO NA KUWAHAKIKISHIA KUWA WATAONESHWA KUWA KWELI HAKUNA MAFUTA KATIKA ENEO HILO. 
 HAPA KATI KATI WANAPO TAZAMA NDIPO KWENYE TANK LA MAFUTA , VIJANA WANANGOJA KUSHUHUDIA. 

Chama Cha Mapinduzi (CCM)Zanzibar:Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ifute Mara Moja Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI)

 Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Mjini Magharibi, Borafya Silima.
---
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimeitaka serikali ya Mapinduzi kuifuta mara moja Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI) kwa kuwa inafanya kazi kinyume na malengo yake usajili.
Kauli hiyo imetolewa jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Mabata huko Magomeni Mjini Unguja na kuhudhuriwa na wanachama wa CCM na wafuasi wa CUF ambapo mgeni rasmi wa mkutano huo alikuwa ni Mwenyekiti wa Mkoa wa Mjini Magharibi Borafya Silima.
Akizungumza katika mkutano huo Katibu wa Vijana wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Mohammed Ali Khalifa alisema chama cha CCM kinamuomba msajili wa taasisi za kiraia achukue uamuzi wa kuifuta jumuiya hiyo ya Uamsho ili isiwepo kabisa katika kumbukumbu za asasi za kiraia hapa Zanzibar.
Alisema taasisi hiyo haiendeshi shughuli zake za kidini licha ya kuwa imesajiliwa kwa misingi ya kuendesha mambo ya dini lakini imepoteza muelekeo na imekuwa ikifanya kazi za kisiasa jambo ambalo linakwenda kinyume na malengo ya jumuiya hiyo.Aidha alisema Uamsho ina mkono wa watu wakubwa ndani ya serikali na ndio muda wote imekuwa ukinyamaziwa na hivyo kuitaka serikali kuwa macho na watendaji wake na kuwachukulia hatua wale wote ambao wamehusika katika kuwaunga mkono na kuwakamta kwa kuwafikisha katika vyombo vya sheria.
Kwa upande wake Mgeni rasmi wa mkutano huo, Borafya Silima alisema jeshi la polisi limefanya kazi nzuri sana ya kuhakikisha linawakamata wahalifu wote na kuwafikisha katika vyombo vya sheria na kuwataka waendelee na kazi hiyo.
Borafya alisema haiwezekani viongozi wa dini ambao hawana elimu kuachiwa kutamba na kuiharibu nchi kwa kisingizio cha kutangaza dini wakati wanachokitangaza ni siasa huku akikishutumu chama cha wananchi CUF kuwa kinahusika moja kwa moja na vurugu zilizotokea kwa kuwabariki viongozi hao wa Uamsho.
“Mtu hana dini yenyewe haijui leo hii tumwite sheikh kwani kuvaa kanzu ndio sheikh? Alihoji huku akishangiriwa na wafuasi wa chama hicho.
Mwenyekiti huyo ambaye amechaguliwa hivi karibuni amesema kwamba nafasi aliyopata ni muhimu katika siasa za Zanzibar na kwamba ataitumia vizuri na kuwataka wapinzani wake wajipange vizuri ili kukabiliana nao kwani wameingizwa madarakani kwa maridhiano.
Borafya alisema Maalim Seif amekuwa amepewa wizara zisizo na uzito wowote serikali na hivyo amekuwa akimuonea choyo makamo wa pili wa rais, Balozi Seif Ali Idd kwa kuwa yeye ndio mshughulikiaji wa wizara zote za serikali.
Mazungumzaji katika mkutano huo ambao kwa kiasi kikubwa wote waliohutubia walimlenga na kumshutumu moja kwa moja Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad na kumtaka aachie ngazi kwa kuwa ameshindwa kutekeleza yale ambao aliapa kuyasimamia wakati akiingia madarakani.
Mbali na matusi ya nguoni na kumshutumu kwamba anahusika na kundi la Uamsho walisema Maalim Seif hafai kuwa kiongozi kutokana na kuwa mbinafsi kwa kuwa ameisema serikali yake mbele ya viongozi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) kwa kuwaeleza kwamba jeshi la polisi na vikosi vya SMZ vinahitaji mafunzo ya kukabiliana na vurugu ili waweze kupata mafunzo ya kukabiliana na vurugu hizo bila ya kuvunja haki za binaadamu.
“Huyu Maalim Seif anawaambia UNDP kwamba jeshi letu la polisi linahitaji mafunzo ya kuwakamata wahalifu sisi tunamwambia polisi wetu na vikosi vyetu havihitaji mafunzo wewe ndio unahitaji mafunzo kwa sababu kwani wewe unalindwa na nani? Si hawa hawa polisi” alisema Khalifa.
Katika hatua nyengine viongozi hao wa CCM walimtaka Maalim Seif kuachia ngazi kwa kwa kumsema rais wake Dk Shein hadharani kitendo ambacho walisema ni kwenda kinyume na kiapo chake cha kuheshimu, kulinda na kutotoa siri za serikali.
Hivi karibuni katika mkutano wake Maalim Seif alimtaka Rais wa Zanzibar Dk Ali Mohammed Shein kutekeleza ahadi yake ya kuwalinda wananchi wote bila ya ubaguzi na kuhakikisha vyombo vya ulinzi vinasitisha ukiukwaji wa haki za binaadamu kwa kuwa wananchi wamechoshwa na ukandamizaji wanaofanyiwa katika nchi yao.
Katibu wa Mufti wa Zanzibar Sheikh Fadhil Soraga Amwagiwa Tindikali na Watu Wasiojulikana

  Katibu wa Mufti wa Zanzibar Sheikh Fadhil Soraga akitolewa katika Chumba cha Huduma ya Mwanzo katika Hospitali ya Mnazi Mmoja baada ya kurushiwa Tindi kali na watu wasiojulikana wakati akifanya mazowezi huko katika Kiwanja cha Mwanakwerekwe.
    Katibu wa Mufti wa Zanzibar Sheikh Fadhil Soraga akipandishwa kwenye Gari ya Wagonjwa kwa lengo la kuwahishwa katika Hospitali ya Muhimbili Dare es Salaam baada ya kurushiwa Tindi kali na watu wasiojulikana wakati akifanya mazowezi huko katika Kiwanja cha Mwanakwerekwe.
Wananchi mbalimbali wakishuhudia Katibu wa Mufti wa Zanzibar Sheikh Fadhil Soraga akiwahishwa katika Hospitali ya Muhimbili Dare es Salaam baada ya kurushiwa Tindi kali na watu wasiojulikana wakati akifanya mazowezi huko katika Kiwanja cha Mwanakwerekwe.Picha na Yussuf Simai-Maelezo Zanzibar

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...

No comments:

Post a Comment