Friday, June 29, 2012

Tunawatambulisha Kwenu Blog maalum ya Miss Utalii Tanzania/Miss tourism Organisation.

Miss Utalii Tanzania, tofauti na mashndano mengine ya urembo, ni zaidi ya shindano la urembo, kwani linalenga katika kutangaza na kuhamasisha Utalii,Utamaduni, Mianya ya Uwekezaji,Elimu,Afya ya Jamii,Utalii wa ndani,Utalii wa kitamaduni,Utalii wa Michezo na Utalii wa Mikitano Kitaifa na kimataifa. Shindano hili pia linahamasisha vita dhidi ya Umasikini,Iharibifu wa mazingira,uwindaji haramu,Uvuvi Haramu,Ujinga,Maradhi, Tamaduni kongwe na Potofu. Miss Utalii Tanzania pamoja na uchanga wake, tangu kuanzishwa kwake mwaka 2005, ni shindano lenye mafanikio makubwa kuliko shindano jingine lolote nchini kitaifa na kimataifa kwani pamoja na kuipa heshima Tanzania ya kuwa wenyeji wa shindano la Dunia la Miss Tourism World 2006, shindano hili ndilo lililo andika historia ya Tanzania kutwaa taji la kwanza la Dunia kabla na baada ya uhuru, pale tulipo twaa taji la Miss Tourism World 2006, pia shindano hili ndilo pekee nchini linashikilia rekodi ya kutwaa mataji ya dunia katika kila shindano tulilo shiriki,tumetwaa mataji 6 ya dunia tangu 2005. Kutokana na mafanikio haya , Tumepewa heshima ya kuaandaa shindano la Dunia la Miss Umoja wa Mataifa mwaka 2013 hapa Tanzania. Ni shindano pekee nchini ambalo washiriki wake hawavai mavazi ya kuogelea, bali mavazi ya heshima yasiyo mdhalilisha mvaaji wala mtazamaji na yaliyo buniwa na kushonwa kwa malighafi za tanzania tu.Link yetu ni : http://www.misstourismorganisation.blogspot.com 


Facebook Page:  https://www.facebook.com/MissUtaliiTanzania


E-Mail:  missutaliitanzania@gmail.com
Asanteni sana.
Miss Tourism Organisation Tanzania.

Deidre Lorenz AMKABIDHI PICHA YA GROUND ZERO RAISI WA MT KILIMANJARO 1991 MARATHON

 Deidre Lorenz akimkabidhi picha ya Ground Zero (New York) Rais wa Mt. Kili Marathon 1991 Onesmo Ngowi baada ya kukimbia mbio hizo
Deidre Lorenz akiwa anahojiwa na waandishi wa Habari mjini Moshi

MWANARIADHA WA KENYA KEMBOI KWA SASA MATATANI



Kemboi anasifika kwa mbio za mita elfu tatu kuruka viunzi na maji. Mwanamke anayedai kufanyiwa kitendo hicho, Anne Njeri Otieno, anadai kuwa mwanariadha huyo alimshambulia wakati alipokataa kuwa na uhusiano wa kimapenzi naye.
Kemboi, aliambia polisi kuwa wakati alipokuwa anamrejesgha nyumbani mwanamke huyo katika mji wa Eldoret, walishambuliwa na watu wlaiokuwa wamejihami na hivyo akajeruhiwa kwenye purukushani hilo.
Kemboi mwenyewe ni afisaa wa polisi na anajiandaa kwenda mjini London kwa michezo ya Olimpiki.
Hata hivyo Kemboi aliachiliwa kwa dhamana baada ya kulipa dola 595 za Kimarekani na kesi yake itasikilizwa tena mwezi Septemba baada ya michezo ya Olimpiki.
"Tayari niko katika kikosi cha wanariadha watakaowakilisha Kenya kwenye michezo ya Olimpiki. Ninaomba mahakama kunipa nafasi niweze kushiriki " alinukuliwa akisema Kemboi mbele ya mahakama.
Mwandishi wa BBC mjini Eldoret Wanyama Chebusiri anasema kuwa Kemboi alichukua muda wa saa saba katika kituo cha polisi alipokuwa anahojiwa.
Kituo hicho cha polisi pia kilijaa watu waliokuwa wanataka kumuona Kemboi alipofika kwa mashtaka.
Hapo awali, Bi Otieno, ambaye anaendelea kupata nafuu hospitalini, aliambia waandishi wa habari kwamba alikuwa kwenye mkahawa mmoja na Kemboi wakati alipokubali kumpeleka nyumbani usiku ulipoingia.
Mwaka 2004 Kemboi aliyeshinda dhahabu kwenye mbio za elfu tatu aliambia polisi kuwa alivamiwa na wezi alipokuwa nje ya gari lake na kumtaka awape pesa na kisha kumshambulia.
Alisema alichukua hatua hiyo ili kujilinda dhidi ya kuvamiwa na katika purukushani hiyo Bi Otieno akajeruhiwa.
chanzo:bbc

Habari Dk. Ulimboka frm Thehabari.com


 BABA wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, mzee Steven Mwaitenda
 Baba wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, mzee Steven Mwaitenda akilia na kufarijiwa
 Usu Mallya akilia baada ya kushuhudia mzee Steven Mwaitenda akibubujikwa na machozi mbele yao
 Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Usu Mallya (kushoto) akiwa na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano, Lilian Liundi walipomtembelea Dk. Ulimboka kumfariji jana
 Mzazi akimlilia mwanaye Dk. Ulimboka kwa uchungu MOI
 Baadhi ya wanaharakati anuai wakiwa na maua walipomtembelea Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Ulimboka kumfariji jana
 Baadhi ya wanaharakati wakiwa na nyoso za hudhuni baada ya kilio cha baba wa Dk. Ulimboka jana MO
Baba wa Dk. Ulimboka aangua kilio MOI
Na Joachim Mushi, Thehabari.com
BABA wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, mzee Steven Mwaitenda amejikuta akiangua kilio kwa uchungu mbele ya wanaharakati ambao walimtembelea mwanae, Dk. Steven Ulimboka kumpa pole kufuatia tukio la kutekwa na kujeruhiwa vibaya na watu wasiojulikana.
Hali hiyo ilitokea jana jioni katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), ambapo wanaharakati kutoka taasisi na asasi mbalimbali za utetezi wa haki za binadamu walifika kwa lengo la kumpa pole Dk. Ulimboka kufuatia kitendo kilichomfika.
Mzee Mwaitenda alijikuta akibubujikwa na machozi na kushindwa kuendelea kuzungumza alipokuwa akitoa shukrani kwa wanaharakati hao, kwa niaba ya mwanaye ambaye wanaharakati hao walishindwa kumuona wote kutokana na hali yake ilivyo sasa.
“Niseme wazi nimefarijika sana kwa ujio wenu kumwona mwanangu dhidi ya mambo ya kikatili aliyofanyiwa akitetea haki za wengine…,” alisema mzee Mwaitenda kabla ya kushindwa kuendelea na kuangua kilio mbele ya wanaharakati.
Baada ya tukio hilo baadhi ya wanaharakati walimshika wakishirikiana na wanafamilia ya mzee Mwaitenda na kumbebeleza kisha kumtoa mbele ya mkusanyiko huo wa wanaharakati na kumrudisha wodini huku wakimfariji.
Wakizungumza mara baada ya tukio hilo wanaharakati wameelezea kusikitishwa na vitendo vinavyoendelea MOI eneo ambalo amelazwa kiongozi huyo wa madaktari ambavyo vimeendelea kutishia usalama wa Dk. Ulimboka.
Akifafanua zaidi mwakilishi wa wanaharakati hao, Markos Albania alisema taarifa walizozipata usiku wa juzi kuna wagonjwa ‘feki’ ambao walijitokeza MOI huku wakitaka kulazwa wodi ya Wagonjwa Mahututi (ICU) alipolazwa Dk. Ulimboka lakini baadaye waligoma kuingizwa wodini.
“Wapo wagonjwa ambao waliletwa na kutaka kupelekwa ICU moja kwa moja…kuna watu wanakuja usiku wa manane wakitaka kumtembelea Dk. Ulimboka…matendo yanayoendelea kutokea ukilinganisha na kauli za Serikali zilizotolewa bungeni yanatishia usalama na uhai wa mgonjwa,” alisema Albania.
Aidha amesema kitendo cha vyombo vya usalama kuendelea kumuhoji Dk. Ulimboka akiwa hoi hospitalini si vya kiungwana kwani tayari muhusika amewataja hadi kwa majina watu ambao anawashuku lakini hadi sasa hakuna aliyechukuliwa hatua yoyote.
Pamoja na hayo wanaharakati hao wameitaka Serikali kuunda tume huru mchanganyiko na raia ambayo itachunguza kiundani suala hilo, kwani hawana imani na Jeshi la Polisi ambalo limedai kuunda timu ambayo inachunguza kwa kina suala hilo.
Dk. Ulimboka ambaye ni kiongozi wa madaktari ambao wanaendelea na mgomo wan chi nzima kuishinikiza Serikali kutekeleza madai yao alitekwa juzi na watu wasiojulikana na kupigwa na kuteswa kikatili kabla ya kutelekezwa katika msitu wa Mabwepande.
*Habari hii imeandaliwa na Mtandao wa Thehabari.com (www.thehabari.com)

MKUTANO WA JUMUIYA YA WASTAAFU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA,ZANZIBAR


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohd Shein akisalimiana na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Zanzibar Mohd Ali Mwalim huko katika mkutano Mkuu wa Wastaafu hao Bwawani Zanzibar.

Rais wa Zanzibar  na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohd Shein akiwahutubia wastaafu wa Jumuiya ya  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Zanzibar  huko katika mkutano Mkuu wa Wastaafu hao Bwawani Zanzibar.
 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohd Shein wakatikati akiwa katika Picha ya pamoja na Viongozi wa Jumuiya ya Wastaafu wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Zanzibar  huko katika mkutano wa Jumuiya hio Bwawani Mjini Zanzibar.


Miongoni mwa Wastaafu wa Jumuiya ya Muungano wa Tanzania wakimsikiliza Rais wa Zanzibar hayupo pichani wakati alipokutana nao huko Bwawani Mjini Zanzibar.

Madaktari Bingwa Nao Wagoma



TUKIO la kutekwa nyara, kupigwa na kujeruhiwa vibaya, kisha kutupwa katika Msitu wa Pande uliopo nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka, limechochea kasi ya mgomo baada ya madaktari bingwa kutangaza kujitosa rasmi kwenye mgogoro huo.Awali madaktari hao hawakushiriki mgomo huo, lakini jana walieleza kwa nyakati tofauti kuwa, wameamua kuungana na wenzao kutokana na unyama aliofanyiwa kiongozi wao akiwa katika harakati za kutetea na kupigania haki zao.

Madaktari hao wa hospitali za Muhimbili, Moi, KCMC, Mbeya, Bugando na Ocean Road ya jijini Dar es Salaam, jana walitangaza rasmi kuwa wameingia kwenye mgomo huo kushinikiza pamoja na mambo mengine, Serikali kutoa tamko kuhusu utata wa tukio hilo.

Tukio hilo la aina yake kutokea nchini, limeathiri upatikanaji wa huduma zote za matibabu katika hospitali hizo, huku madaktari katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na Moi, wakielekeza nguvu zao kunusuru maisha ya mwenzao aliyeumizwa.

Katibu wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Edwin Chitage, aliwaambia waandishi wa habari kuwa mgomo huo utaendelea hadi hapo Serikali itakapotekeleza madai yao.

"Tunaitaka Serikali kuacha vitisho kwa madaktari nchini, tunaitaka itambue kwamba mgogoro huu hauwezi kumalizwa kwa njia yoyote vikiwemo vitisho bali ni kwa kukaa meza ya majadiliano na kukubaliana na madaktari," alisema Dk Chitega na kuongeza:

"Ninawashukuru madaktari wote nchi nzima, wauguzi na wafanyakazi wa sekta ya afya kwa ujumla wao kwa kusitisha huduma baada ya kupigwa mwenzetu. Tunaomba mshikamano huu uendelee," alisema Dk Chitega.

Gazeti hili lilishuhudia wagonjwa wakiwa wamekaa katika makundi bila kujua la kufanya, huku wengine wakiamua kuondoka na kwenda hospitali binafsi.

Waliliambia Mwananchi kwamba kitendo alichofanyiwa Dk Ulimboka ni cha kinyama na kuungana na madaktari hao kuitaka Serikali kutatua mgogoro huo haraka.

Wagonjwa waliofika katika eneo hili pia walielezwa bayana na maofisa wa Moi kwamba huduma zimesitishwa kutokana na madaktari kugoma.

Ocean Road

Madaktari bingwa katika Taasisi ya Ocean Road nao waligoma kutoa huduma hatua iliyozua taharuki kwa wagonjwa waliofika kwa ajili ya matibabu.

Gazeti hili lilishuhudia ofisi za madaktari hao zikiwa zimefungwa na hata zile ambazo zilikuwa wazi, madaktari hawakuwapo.

Mmoja wa wagonjwa aliyejitambulisha kwa jina la Joyce Dachi, alisema kuwa, wagonjwa wengi wamekuwa wakiandikishwa mapokezi, lakini wanachukua muda mrefu kumuona daktari.


Mgomo huo pia umeendelea katika Hospitali ya Amana wilayani Ilala huku uongozi wa hospitali hiyo ambao uligoma kuzungumza na vyombo vya habari, ukihaha kunusuru hali hiyo.

Katika Hospitali za Temeke na Mwananyamala huduma ziliendelea kutolewa kama kawaida.

Mbeya

Katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya ,madaktari bingwa ambao awali hawakugoma jana waliingia kwenye mgomo na kusababisha wagonjwa katika hospitali hiyo hususan kitengo cha wazazi, kusota bila matibabu.

Habari kutoka katika hospitali hiyo zilieleza kuwa hivi sasa madaktari bingwa wanatoa huduma kwa kujuana.

Mmoja wa madaktari hao ambaye hakutaka kutajwa gazetini, alisema kitendo alichofanyiwa Mwenyekiti wa Jumuiya yao kimewakatisha tamaa.

Alisema kuwa, hali hiyo sasa imehamia hadi katika Kituo cha Wazazi cha Meta na kufafanua kuwa hali ni mbaya, tayari wajawazito wametakiwa kuhamia katika Hospitali ya Mkoa ambayo imefurika wagonjwa.

Mkurugenzi wa Hospitali hiyo ya Rufaa, Dk Eliuter Samky hakuweza kuzungumzia tukio hilo jana kutokana na kile kilichoelezwa na katibu wake muhtasi kwamba ana kazi nyingi.

Mwanza
Madaktari katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando (BMC) mkoani Mwanza nao wamegoma, huku kiongozi wa Kamati Ndogo ya hospitali hiyo inayoshughulikia migomo, akikataa kuzungumzia hali hiyo.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu baada ya kutoonekana katika maeneo ya hospitali, mmoja wa viongozi wa Kamati hiyo, Dk Geogre Adrian, alisema kwa sasa hawezi kulitolea ufafanuzi suala hilo na kwamba kufanya hivyo, ni kwenda kinyume na maagizo aliyopewa na Kamati Kuu.


Akizungumzia huduma katika hospitali hiyo alisema kuwa hajui lolote kwa kuwa hawajagusa maeneo ya kazi kwani wapo kwenye mgomo.

Kaimu Mkurugenzi wa hospitali hiyo alipotafutwa kwa njia ya simu ili kuzungumzia huduma katika hospitali yake, hakupatikana.

Watimuliwa
Jana Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk Charles Majinge alitoa tangazo la kuwataka madaktari waliopo mafunzoni ‘Interns’ katika hospitali hiyo kurejea kazini na kama watakiuka agizo hilo, watakuwa wamejifukuzisha wenyewe.


Manyara
Mkoani Manyara, madaktari kumi katika Hospitali ya Haydom Wilaya ya Mbulu wamegoma tangu juzi.Idadi ya wagonjwa katika hospitali hiyo inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), inaongezeka siku hadi siku.

Wakizungumza na waandishi wa habari kwa masharti ya kutotaka kutajwa majina yao, madaktari hao ambao wanafanya mafunzo ya vitendo katika hospitali hiyo, wamesema kuwa hawatatibu wagonjwa mpaka madai yao yatekelezwe.


Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Anatory Choya, alithibitisha kutokea kwa mgomo huo na kufafanua kwamba wanaendelea kufanya mazungumzo ili kupata ufumbuzi.

Choya alisema kuwa madaktari wanaoendelea na kazi, wameelemewa kutokana na wagonjwa kuwa wengi.

Alisema kati ya madaktari 11 wanaosoma kwa vitendo hospitalini hapo, mmoja tu anayesomeshwa na hospitali hiyo, ndiye hajagoma.

KCMC
Hali katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC mkoani Kilimanjaro imezidi kuwa tete na kuwafanya ndugu kuwahamishia wagonjwa wao katika hospitali binafsi.

Mwananchi lilitembelea wodi za hospitali hiyo na kukuta vitanda vikiwa wazi.

Wakizungumza na gazeti hili, baadhi ya madaktari ambao wapo kwenye mgomo kwa sharti la kutotajwa majina, walisema hawako tayari kurudi kazini kwa kuhofia usalama wa maisha yao.

Dodoma
Wagonjwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma jana walijikuta wakipata taabu baada ya madaktari wa hospitali hiyo kusitisha huduma kwa takriban saa sita kuanzia asubuhi.

Muda wa mchana utoaji huduma katika hospitali hiyo uliendelea ingawa kwa kusuasua.

Tofauti na siku zote, jana chumba cha daktari kilichokuwa wazi ni kimoja tu hali iliyosababisha msongamano mkubwa.

Arusha

Mjini Arusha, madaktari wameendelea na mgomo katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru na kusababisha kudorora huduma huku wagonjwa kadhaa wakiondolewa hospitalini hapo.

Mgomo huo, ulianza saa 1 asubuhi hadi saa 6:00 mchana, ambapo madaktari na wauguzi,waligoma kutoa huduma wakitaka kujua hatima ya Dk Ulimboka. Walitaka pia kuzungumza na uongozi wa hospitali hiyo na waandishi wa habari, kuhusu mgogoro wao.

Askari anyimwa huduma
Askari wa Usalama Barabarani ambaye jina lake halikufahamika mara moja ambaye alipata ajali jana, alijikuta akishindwa kuhudumiwa katika hospitali ya Mount Meru na kuondolewa kutokana na mgomo huo.

Askari huyo, aliyevaa sare, alifikishwa hospitalini hapo saa 5:00 asubuhi akiwa kwenye teksi, lakini wauguzi waliokuwa zamu walishauri apelekwe sehemu nyingine.

Hata hivyo, uongozi wa hospitali ya mkoa, ukiongozwa na Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk Omar Chande, jana ulifanya kazi ya ziada ya kuwabembeleza madaktari hao, kurejea kazini, kusubiri uamuzi wa Serikali.

Mgomo, Dk Ulimboka vyateka Bunge

Mgomo wa madaktari na kutekwa kisha kupigwa Dk Ulimboka jana vilitawala mjadala wa Bunge hadi pale Spika Anne Makinda alipotoa mwongozo kwamba suala hilo lisijadiliwe kwani liko mahakamani.

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alilazimika kutoa ufafanuzi wa hoja yake aliyoitoa juzi pale alipokuwa akizungumzia mgomo wa madaktari na kuhitimisha kwamba Serikali ilikuwa inajiandaa kutoa kauli na msimamo wake hivyo “liwalo na liwe’.

Pinda alilazimika kutoa maelezo kutokana na swali aliloulizwa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe aliyetaka kufahamu maana ya kauli ya Waziri Mkuu ambayo aliita kuwa ni nzito na iliyozua mjadala mkali nchini.

Kadhalika, Mbowe alitaka kufahamu hatua ambazo Serikali imechukua kuhakikisha kwamba wananchi wanaendelea kupata huduma za tiba kutokana na kuwapo kwa taarifa kwamba madaktari katika hospitali kadhaa walikuwa wakiendelea na mgomo.

Kadhalika Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alimuuliza Pinda kwamba haoni kwamba ni busara kujiuzulu wadhifa wake kutokana na ahadi yake kwamba mgomo wa madaktari usingetokea, lakini ahadi hiyo imeshindwa kutekelezeka.

Akimjibu Mbowe, Pinda alikiri kutoa kauli hiyo ndani ya Bunge juzi na kusema alifanya hivyo akiamini kuwa jambo hilo lilikuwa mahakamani na akasema asingeweza kusema jambo lolote kwa kuwa hana tabia ya kuwa na utovu wa nidhamu wa kuingilia mambo ya mahakamani.

Hata hivyo, alijitetea kuwa kabla ya kutoa kauli hiyo bungeni juzi, hakuwa na taarifa kuhusu tukio la kupigwa kwa Ulimboka na akasema kuwa, kauli yake haihusiani kabisa na Serikali kuhusika katika jambo hilo kwa namna yoyote ile.

Waziri Mkuu alisema tayari amekwishaagiza vyombo husika kufanya uchunguzi wa kina na kutoa majibu ya haraka ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua stahiki mara moja.

“Kwanza namtakia afya njema ndugu Ulimboka, na mimi nataka Watanzania waamini kuwa tulikuwa katika mazungumzo mazuri na madaktari chini yake Ulimboka hivyo tukio hilo ambalo limetokea katika mazingira magumu limetushtua kweli, kama ni Serikali basi ingekuwa ni Serikali ya ajabu kweli,’’alisema Pinda.

Kuhusu namna ya kusaidia Watanzania wasiathirike na mgomo huo, alisema tayari Serikali imeshaagiza madaktari kutoka wizarani kutumika na kuwaomba waliostaafu kutoa huduma katika kipindi hicho kigumu.

Mkakati mwingine ni pamoja na kutumia hospitali za Jeshi ikiwamo Lugalo waanze kutoa huduma hizo wakati Serikali inaendelea kuzungumza kwa utaratibu na madaktari.

Lissu aliuliza swali la nyongeza kumtaka Pinda kuachia ngazi hali iliyosababisha mvutano kwani Waziri Mkuu alikosoa uulizaji wa swali hilo kuwa halikustahili.

Baada ya kipindi cha maswali na majibu, Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika aliomba mwongozo wa Spika kuhusu suala la madaktari akitaka taarifa ya Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii ambayo ilifanyia kazi suala la mgomo wa madaktari ijadiliwe bungeni.

Hata hivyo, Spika Makinda alisema ripoti hiyo haiwezi kujadiliwa kwani tayari Serikali ilishakabidhiwa kwa ajili ya kuifanyia kazi na kwamba mapendekezo ya Bunge kupitia ripoti hiyo yamefanyiwa kazi kwa kiasi kikubwa.

Habari hii imeandaliwa na Neville Meena na Habel Chidawali, Dodoma, Godfrey Kahango,Mbeya, Joseph Lyimo,Mbulu, Sheilla Sezzy,Mwanza, Rehema Matowo, Moshi, Masoud Masasi,Dodoma, Fidelis Butahe, Geofrey Nyang'oro Dar, Mussa Juma, Arusha, Bakari Kiango na Victoria Mhagama.

NMB YAFUNGUA TAWI TEGETA


NMB inaendelea kupanua mtandao wake wa matawi na kusogeza huduma zake karibu na wateja wake. Sasa NMB ipo katika eneo la Tegeta  katika jengo la Kibo Commercial Complex, Tegeta Kibaoni.
NMB ndiyo benki ya kwanza yenyematawi mengi na ATM nyingi zaidi nchini, imekuwa kinara katika ubunifu Tanzania kwa kuanzisha akaunti mpya nyingi na ndiyo benki ya kipekee iliyopo takribani kwa asilimia 95 ya wilaya zote nchini.

Wateja wa Benki ya NMB wakipata huduma katika Teller za benki hiyo iliyopo Tegeta Jengo la Kibo Commercial Complex Tegeta Kibaoni



NMB ni Full Mzuka.
You might also like:

Thursday, June 28, 2012

DEIDRE LORENZ KAINGIA KWENYE MAPENZI NA TANZANIA



Mcheza sinema maarufu wa Marekani Deidre Lorenz ameahidi kuleta wacheza sinema wenzake na kushiriki kwenye mbio za mwaka kesho za mt. Kilimanjaro Marathon zitakazokuwa zinatimiza miaka 23 tangu zianzishwe mwaka 1991.
 
Lorenz aliyekimbia mbio za mwaka huu ambazo zilipewa jina la “mbio za kutimiza miaka 50 ya uhuru wa Tanganyika” na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) amesema kuwa atakuja na timu yake ya wapiga picha ili kupiga picha vivutio kadhaa vya Tanzania ikiwa ni pamoja na mlima Kilimanjaro. Qwiji hili la sinema za Santorini Blue, The Great Fight, Perfect Strangers na nyingine nyingi ameelezea kuipenda sana Tanzania.

“Sikutegemea kuikuta nchi nzuri kama hii” alisema mcheza sinema huyo ambaye ameshawahi kuchaguliwa zaidi ya mara 4 kugombea tuzo maarufu za Oscar. “Sasa nimeamini kuwa mlima Kilimanjaro ni mali ya Tanzania na nitautangaza katika sinema zangu zote” aliendelea kusema Deidre Lorenz.

Mcheza sinema huyu ambaye ameingia kwenye mkataba na kampuni kubwa ya Google hivi karibuni ili kuuza sinema zake katika mtandao aliielezea Tanzania kama nchi nzuri na yenye watu wakarimu sana.

Mbio za Mount Kilimanjaro Marathon zilianzishwa mwaka 1991 na Marie Frances anayetoka katika jiji la matajiri la Bethesda nchini Marekani baada ya kuombwa na balozi wa zamani wa Tanzania nchini Misri. Tangu kuanzishwa kwake mbio hizi zimekuwa zinaleta watalii matajiri katika mji wa Moshi kupanda mlima Kilimanjaro na kukimbia mbio hizi zinazojulikana kama Seven Continental Races.
 
Hakuna masharti yote ya kukimbia mbio hizi na watanzania wanaoshiriki katika mbio hizi huwa hawatozwi pesa za kiingilio.
 
Kwa kutambua mchango wake katika uchumi wake Manispaa ya Moshi iliibadilisha jina barabara ya zamani ya Bustani Ale na kuiita Marie Frances Boulevard ili kumuenzi mama huyu aliyejitolea maisha yake kuutangaza mlima Kilimanjaro.

“Kila siku napokea ujumbe kutoka nchi mbalimbali niende huko kuanzisha mbio za marathon lakini kwa sasa basi” alisema mama huyo aliyekuwa mtayarishaji wa vipindi vya televisheni ya ABC kabla ya kunzisha Mt. Kilimanjaro Marathon.
 
Alisema kuwa mwaka jana yeye na Rais wa klabu ya Mt. Kilimanjaro Marathon mtanzania Onesmo Ngowi walifanya makubaliano ya Ethiopia Airlines (ET) jijini Addis Ababa kuzifanya mbio hizo kuwa za kimataifa zaidi. “ET walikubali kutoa ufadhili kwetu na pia kugharamia kushiriki kwetu katika mbio za New York Marathon, Boston Marathon na Los Angelos Maratthon ili kuitangaza vyema Tanznaia” alibainisha Frances.
 
Katika makubaliano hayo, Ngowi na Frances pia wataanzisha mbio za “King Solomon Marathon” zitakazofanyika katika jiji la Addis Ababa nchini Ethiopia.
 
Deidee Lorenz amefungua pazia kwa watu mashuhuri kushiriki katika mbio za marathon nchini Tanzania na ni jukumu la Watanzania kuchangamkia fursa zinazoletwa na ujio wao.

Imetumwa na:

Grace Soka

Afisa Uhusiano


                                  MT. KILIMANJARO MARATHON 1991


RAY AZINDUA FILAMU YA SOBING SOUND KWA KUTOA MSAADA AKISHIRIKIANA NA STEPS

Msanii wa filamu nchini Vicent Kigosi 'Ray' akikabizi sehemu ya msaada uliotolewa na Kampuni ya Steps Entatainment ya jijini Dar es salaam leo kwa Mlezi wa kituo cha Maunga Centre   kilichopo Kinondoni Zainabu Bakari vyakula mbalimbali vimetolewa vyenye samani ya shilingi milioni moja na nusu katika kituo hicho kushoto ni Meneja Masoko wa Kampuni ya Steps, Ignatus Kambarage
Msanii wa filamu nchini Vicent Kigosi 'Ray' akikabizi sehemu ya msaada uliotolewa na Kampuni ya Steps Entatainment ya jijini Dar es salaam leo kwa Mlezi wa kituo cha Maunga Centre   kilichopo Kinondoni Zainabu Bakari vyakula mbalimbali vimetolewa vyenye samani ya shilingi milioni moja na nusu katika kituo hicho kushoto ni Meneja Masoko wa Kampuni ya Steps, Ignatus Kambarage
Msanii wa Filamu Nchini Visent Kigosi 'Ray' katikati na Meneja Masoko wa Kampuni ya Steps.Ignatus Kambarage wakiwa katika picha ya pamoja baada ya lei kugawa vyakula mbalimbali katika kituo cha kulelea watoto yatima cha Maunga Centre vilivyotolewa na Kampuni ya Steps wakati wa Uzinduzi wa filamu yao Mpya ya Sobing Sound.
  
MSANII wa filamu nchini  Visent Kigos 'Ray'  amezindua filam yake  mpya inayojulikana kama 'SOBING SOUND'.

Filam hiyo ameizindua kwa staili tofauti ambapo badala ya kuzindua Ukumbini kama ilivyozoeleka na wengi, msanii huyo amezindua filam hiyo katika kituo cha watoto yatima cha Maunga Centre kwa kutoa msaada wa vitu mbalimbali vyenye thamani ya sh. milioni 1.5  kwa niaba ya Kempuni ya Steps Entatainment ya jijini Dar es salaam

Akizungumza mara baada ya kuzindua filamu hiyo akiwa pamoja na watoto yatima wa kituo hicho, Ray alisema ameamua kufanya hivyo kutokana na ukweli kwamba  watu wengi wamekuwa wakifurahia maisha uku wengine wakiendelea kutahabika kitendo ambacho si kizuri.

Alisema ujio wa filamu hiyo ni kama azma yake aliyoipanga tangu awali kuhakikisha filamu zake zote zinafanya vizuri na atakuwa kila filamu anayotoa atakikisha japo kidogo kwa namna yoyote anawakumbuka watoto yatima kwana awajapenda.


Alisema msaada uliotolewa kwa watoto yatima hautaishia kwao bali ataendelea kutoa kile atakachokipata kupitia filamu hiyo kuwasaidia na wale wasiojiweza amesema kampuni ya  Steps Entertaiment imekuwa msaada mkubwa kwa wasanii kutambulika na kutushawishi tuwe tunawakumbuka watoto wanaoishi katika mazingila magomu.


Nae mmoja wa wakilishi wa Kampuni ya Steps Ignatus Kambarage amesema swala la watoto yatima ni letu sote na wala alichagui kwa kuwa tunawajibu na angalau kidogo tunachokipata kupitia filamu zetu tunarudisha kwa kutoa shukrani zetu.


tamasha la serengeti fiesta 2012 lazinduliwa rasmi jijini dar

Mmoja wa Waratibu wa maandalizi ya tamasha la Serengeti Fiesta 2012 (pili kulia) Sebastian Maganga  akifafanua baadhi mambo mbele ya wageni waalikwa wakiwamo wanahabari kutoka vyombo mbalimbali wakati wa uzinduzi rasmi wa tamasha hilo uliofanyika kwenye viwanja vya Lidaz Club,Kinodoni jijini Dar leo,tamasha hilo linatarajia kutimua vumbi zake hivi karibuni katika mikoa mbalimbali,ambapo katika tamasha hilo mdhamini mkuu ni kampuni ya bia ya Serengeti kupitia bia yake ya Serengeti Premium Lager,Kampuni ya mafuta ya Gapco pamoja na Push Mobile.Kauli mbiu ya tamasha hilo ni "MUONEKANO MPYA-BURUDANI ILELE-BAAAS"!
Sehemu ya zawadi mbalimbali zitakazotolewa kwenye tamasha la Serengeti Fiesta 2012,ikiwemo Magari aina ya Toyota Vitz kila moja lenye thamani ya shilingi milioni nane,Piki piki a.k.a Boda Boda 14 kila moja ikiwa na thamani ya shilingi milioni moja na nusu na zawadi nyingine zikiwemo simu aina ya blackberry,Nokia.
Baadhi ya Wadau mbalimbali wa tamasha la Serengeti Fiesta 2012 wakishuhudia uzinduzi huo uliofanyika kwenye viwanja vya lidaz Club,jijini dar.
Mmoja wa waratibu wa tamasha la Serengeti Fiesta 2012,Sebastian Maganga akifafanua  jambo kwa umakini na kuweka  msisitizo kwa Wanahabari waliofika kwenye uzinduzi wa  tamasha hilo.
Sebastian Maganga kutoka Clouds Media Group akiwatambulisha Wadhamini wa tamasha la Serengeti Fiesta 2012,Kutoka kulia ni Mkuu wa Masoko wa kampuni ya mafuta ya Gapco,Ben Temu,Meneja wa kinywaji cha Serengeti kutoka SBL,Allan Chonjo pamoja na muwakilishi wa kampuni ya Push Mobile,Bw.Rodney
Meneja wa bia ya Serengeti kutoka kampuni ya SBL,ambao ndio wadhamini wakuu wa tamasha la Fiesta 2012,Allan Chonjo akizungumza machache mbele ya wageni waalikwa wakiwemo wanahabari kutoka vyombo  mbalimbali,uliofanyika leo kwenye viwanja vya Lidaz Club,jijin Dar.
Bw.Rodney ambaye ni muwakilishi wa kampuni ya Push Mobile akionesha moja ya namba zitakazotumika kutoa taarifa mbalimbali za tamasha hilo litakaloanza kutimua vumbi zake kuanzia hapo kesho katika mikoa ya Arusha na Mbeya na baadaye mikoa mingine.
Pichani shoto ni Meneja mahusiano ya ndani ya kampuni ya bia ya Serengeti,Bw.Iman Lwinga akiwa sambamba na baadhi ya wanahabari waliofika kwenye uzinduzi wa tamasha la Serengeti Fiesta 2012.
Wageni waalikwa wakiwemo wasanii kadhaa pia walifika kushudia tukio hilo kubwa la kihistoria katika tasnia ya burudani hapa nchini.
 Wakifuatilia kwa umakini zaidi.
Kwa mshangao mkubwa wakishuhudia uzinduzi wa tamasha la Serengeti Fiesta 2012 ndani ya viwanja vya Lidaz Club.
 Wadau wakifuatilia uzinduzi huo,akiwemo Shaffih Dauda mzee wa sports bar.
 Meneja wa vinywaji vikali wa SBL,Bw.Emillian Rwejuna akizungumza na Meneja wea kinywaji cha Serengeti Premium Lager,Allan Chonjo wakati wa uzinduzi wa tamasha la Serengeti Fiesta 2012.
 Mtangazaji wa Clouds FM,Millard Ayo akifanya mahojiano mafupi na msanii wa muziki wa kizazi kipya,Mwasiti kuhusiana na tamasha la fiesta kwa ujumla.
Wadadazi nao walikuwepo kunogesha uzinduzi huo wa tamasha la Serengeti Fiesta 2012.

HAPO VIPI...HAPO SAWA...

Ofisa wa Polisi akimzuia mpiga picha wa gazeti la Tanzania Daima, Francis Dande, asimpige picha wakati wakimuondoa askari mwenzao aliyeshambuliwa na madaktari akituhumiwa kukutwa akipiga simu ya kuwataarifu wenzake kuwa Dk. Ulimboka hakufa.

PROFESA LIPUMBA KWENDA KUMJULIA HALI DK ULIMBOKA LEO HII

Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wananchi, Profesa Ibrahim Lipumba (kulia), leo saa 10 jioni atakwenda kumtembelea kumjulia hali, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Stephen Ulimboka ambaye amelazwa kwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jana baada ya kutekwa na kupigwa na watu wasiojulikana.Picha Na Richard Mwaikenda Blog

MATUKIO YA WAZIRI MKUU PINDA BUNGENI DODOMA

 Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza na Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed (kushoto) na Mbunge wa Viti Maalum, Leticia Nyerere kwenye viwanja vya Bunge Mjini Dodoma Juni 27,2012.
 Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akizungumza na Mbunge wa Mbinga Mashariki Gaudence Kayombo, kwenye jengo la utawala la Bunge Mjini Dodoma Juni 27,2012.
 Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akisalimina na Mbunge wa Dole, Sylvester Mabumba kwenye viwanja vya Bunge Mjini Dodoma  Juni  27, 2012.
 Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akisalimiana  na wawekezaji katika sekta ya madini mkoani Mara kutoka kampuni ya Gemini Corporation ya Urusi baada ya kuzungumza nao, Ofisini kwake  Bungeni  Mjini Dodoma Juni 27,2012. Kushoto ni Mwenyeji wao , Mbunge wa Viti Maalum Zainab Kawawa.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akiwa katika picha ya pamoja na wawekezaji katika sekta ya madini mkoani Mara kutoka kampuni ya Gemini Corporation ya Urusi baada ya kuzungumza nao, Ofisini kwake  Bungeni  Mjini Dodoma Juni 27,2012. Kushoto ni Mwenyeji wao , Mbunge wa Viti Maalum Zainab Kawawa. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Redds Miss Mara 2012

Washiriki wa shindano la Redds Miss Mara 2012 wakiwa katika picha ya pamoja katika ufukwe wa Ziwa Victoria, mkoani Mara baada ya mazoezi yao jana. Warembo hao wanataraji kupanda jukwaani Ijumaa, Juni 29, 2012 kuchuana vikali kuwania taji la mkoa wa mara na tiketiketi ya Kushiriki shindano la Redds Kanda ya Ziwa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,Balozi Seif Iddy Akutana na Mwakilishi wa Taasisi ya Huduma za Teknolojia ya Afya ya Chuo Kikuu Cha Brown Kilichopo Boston Nchini Marekani

Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Balozi Seif Iddy akimsalimia mwakilishi wa Taasisi ya Huduma za Teknolojia ya Afya ya Chuo Kikuu Cha Brown kilichopo Boston Nchini Marekani Bw. Jayson ofisini kwake Vuga mjini Unguja, Zanzibar. Katikati ni Mkurugenzi mwenza wa Taasisi hiyo Bwana Hai Sheng Chia. 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizungumza na Mwakilishi wa Taasisi inayojihusisha na  huduma za Teknolojia ya Afya Nchini Marekani ya Med International Bwana Jayson Marwaha ambaye wapo Nchini kufanya utafiti wa Afya kwa Hospitali za Zanzibar. Hatua hii ni utekelezaji wa ahadi waliyompa Balozi Seif wakati walipokutana nao Nchini Marekani Mwezi Oktoba Mwaka jana.Kulia Kwa Balozi Seif ni Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Dr. Sira Ubwa Mwamboya.Picha na Saleh Masoud-Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

Mgogoro Wa Serikali Na Madaktari Ni Balaa Kwa Taifa

Waziri Mkuu Mizengo Pinda akisalimiana na Mwenyekiti wa Jumuia ya Madaktari nchini Dk Stephen Ulimboka wakati Waziri Mkuu Mizengo Pinda alipokutana na Madaktari Jijini Dar  es Salaam
--
Ndugu zangu,

Nimepitia nilichoandika Februari 4, 2012 juu ya mgogoro wa madaktari na Serikali nikaona ni vema niyarushe tena maandiko yangu yale kama yalivyokuwa, bila kuongeza au kupunguza neno. Maana, kuna ambacho wahusika wanaweza hawakukiona wakati ule, lakini wakakiona sasa. Soma nilichoandika...

Ndugu zangu,

Mgomo wa madaktari wetu ni habari kubwa. Umeingia sasa kwenye wiki ya pili. Hata kama ungekuwa ni wa siku mbili, bado ungesababisha madhara makubwa kwa nchi. Kwamba sasa una zaidi ya siku kumi na nne ni balaa kubwa kwa nchi yetu.

Tafsiri yangu;

Uliopo ni mgogoro kati ya madaktari na Serikali. Na kwenye mgogoro kama huu, siku zote, wenye kuathirika zaidi ni wananchi walio wengi.

Ni ukweli, kuwa karibu kila Mtanzania anayeamka asubuhi, ama ni mgonjwa au ana ndugu, jamaa au rafiki aliye mgonjwa.

Hivyo basi, kuna mamilioni ya Watanzania wenye kutaabika kila siku na maradhi ya aina mbali mbali. Ni Watanzania wenye kutegemea sana huduma ya tiba inayotolewa na madaktari wetu. Na katika nchizetu hizi, daktari ni rafiki muhimu sana wa mwananchi.

Ni jambo baya sana, pale Serikali inapoingia kwenye mgogoro na madaktari. Inapoingia kwenye mgogoro na marafiki wa wananchi. Hakuna mahali popote duniani wananchiwakatokea kuwachukia madaktari.

Hivyo basi, ni balaa pia pale Serikali inaposhindwa kumaliza tofauti zake na madaktari wa wananchi kwa njia ya mazungumzo na hata kufikia hatua ya madaktari kugoma.

Katika nchi zetu hizi, mganga wa tiba aliyesomeshwa kwa fedha za walipa kodi na kwa miaka mingi anahitajika sana. Mganga wa tiba msaidizi anahitajika sana. Na hata kama angelikuwapo Msaidizi wa Mganga Msaidizi wa tiba , naye angehitajika sana. Vivyo hivyo kwa wakunga wakuu na wasaidizi, wauguzi wakuu na wasaidizi wao. Wote hao anahitajika sana.

Na katika nchi zetu hizi, Serikali hazipaswi kufikia hatua ya kuwatisha na hata kuwafukuza kazi madaktari. Hilo la mwisho lifanyike tu pale ambapo njia nyingine zote za kumaliza tofauti na kusuluhisha migogoro na madaktari zitakapokuwa zimeshindikana. Na kwanini ishindakane?

Tufanye nini sasa?

Taarifa kwamba Kamati ya kudumu ya Bunge inayohusika na masuala ya huduma za jamii imepanga kukutana na madaktari wetu ni hatua njema na ya busara. Maana, katika mgogoro huu taarifa zimekuwa zaidi za upande mmoja; upande wa Serikali. Ni wakati sasa pande zote mbili zikasikilizwa na Kamati hiyo ya Bunge. Ndio, ni wakati pia hata madaktari wetu wakapewa nafasi tuwasikie.

Huu si wakati wa kufanya "propaganda" za kisiasa kwenye masuala ya afya za wananchi. Na hata pale Waziri wa Afya alipokaririwa jana Bungeni akitamka kuwa hali ya huduma za mahospitalini zimerejea katika hali yake ya kawaida ni mfano wa ’ Propaganda’ za kisiasa ambazo Watanzania hatuzihitaji kwa sasa.

Hivi ni hali gani hiyo iliyorejea kwenye kawaida yake kwenye hospitali zetu baada ya mgomo huu wa madaktari unaoendelea sasa? Kwamba askari wetu wa Jeshi la Wananchi wamelazimika kwenda kutibu wagonjwa Muhimbili hiyo haiwezi kuwa ni ’ Hali ya kawaida’. Kwamba madaktari wameripoti lakini hawaonekani mawodini hiyo haiwezi kuwa ’ hali ya kawaida’. Na kama ni kawaida, hivi ni nini tafsiri ya ’ kawaida’?

Hapa kuna ukweli unaopaswa kusemwa, na si kitu kingine bali ni ukweli. Watanzania tunataka kujua; ni kwanini watendaji wa Wizara husika wameshindwa kulitatua suala la madaktari wetu na hata kutufikisha hapa tulipo?

Yumkini, kulikuwa na hali ya kuyapuuzia madai ya madaktari katika hatua za awali. Yawezekana pia watendaji wa Wizara hawakuwa karibu na wawakilishi wa madaktari hao ili kutoa fursa ya kuongea na kutafuta ufumbuzi wa tatizo. Labda ndio maana tumefika mahali sasa mgogoro umekomaa na wahusika kuonyesha hali ya kutunishiana misuli.

Kuna mahali kosa limefanyika. Ni wapi?

Ndio hapa, kuwa hata kama Kamati ya Bunge itafaulu kusuluhisha mgogoro huu, bado Watanzania tutahitaji iundwe Tume huru itakayochunguza namna watendaji wa wizara husika walivyolishughulikia suala hili kwa upande wao.

Tume hiyo itusaidie kuupata ukweli mzima ili kama taifa, tujifunze. Na wakati tume kama hiyo itakapokuwa ikifanya kazi yake, itakuwa ni busara, kwa watendaji wakuu wa wizara husika wajiweke pembeni kwa maana ya kujiuzulu ili kupisha uchunguzi huo.

Kama Tume itabaini kuwa hakukuwa na mapungufu makubwa katika utendaji wao na hususan walivyolishughulikia suala hili la mgogoro na madaktari, basi, itajulikana hivyo, na wana nafasi ya kurudi tena kwenye nafasi za utendaji Serikalini. Inahusu umma kurudisha imani yake kwa Serikali yao. Ndio maana ya umuhimu wa wahusika kupisha pembeni kuruhusu uchunguzi ufanyike. Maana, haitakuwa busara kuliacha suala hili likapita kama yanavyopita mengine ilihali limegharimu maisha ya Watanzania.

Na kubwa zaidi kwa sasa, ni kwa pande zote katika mgogoro huu kutambua; kuwa kwa sasa mvutano unaoendelea hautatoa mshindi, ni kwa vile, katika kilichotokea na kinachoendelea kufanyika sasa, sote, kama taifa, tumeshindwa.

Huu ni wakati wa kutanguliza busara na hekima. Tufanye yote, lakini, njia mujarab ya kutanzua mgogoro huu uliopo sasa ni mazungumzo katika mazingira ya kuheshimiana, basi.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.

Maggid Mjengwa,

Dar es Salaam,
Jumamosi, Februari 4, 2012