Saturday, January 19, 2013

Kutoka Kwa Mbunge wa Jimbo la Ubungo-CHADEMA,John Mnyika:'Rais na Mawaziri wanadharau wabunge kuhusu mabadiliko ya mzunguko wa Bajeti.'



 
 Mbunge wa Jimbo la Ubungo-CHADEMA,Mh John Mnyika
---
 
Yaliyojiri na yanayoendelea kujiri ndani ya Baraza la Mawaziri na Wizara ya Fedha kuhusu mabadiliko ya mzunguko na mchakato wa bajeti yanaashiria kwamba Rais na Serikali wanadharau mamlaka na madaraka ya Bunge na wabunge.

Aidha, kutokana na umuhimu wa mzunguko na mchakato wa bajeti katika kuwezesha uwajibikaji kwenye mapato na matumizi ya rasilimali za umma; Waziri wa Fedha anatakiwa aweke wazi kwa umma mabadiliko hayo yaliyofanyika ili wananchi na wadau waweze kutoa maoni na Bunge liweze kuyazingatia wakati wa marekebisho ya kanuni za Bunge yanayotarajiwa kufanywa katika mkutano wa kumi wa Bunge.

Wakati Katibu wa Bunge amenukuliwa tarehe 17 Januari 2013 akisema kwamba pendekezo la mabadiliko ya mzunguko na mchakato wa bajeti bado linajadiliwa na kwamba iwapo litaafikiwa, uamuzi utatangazwa mapema mwezi ujao (Februari 2013) wakati wa mkutano wa Bunge; upande wa Rais na Wizara ya Fedha wameshapitisha na kuanza kutekeleza mzunguko na mchakato mpya wa bajeti kuanzia mwezi Disemba 2012.

Kwa upande wangu nitashiriki vikao vya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha na Uchumi wiki ijayo ili nipate mwanya wa kumhoji Waziri wa Fedha kwa kurejea matakwa ya Katiba ya Nchi, Sheria ya Fedha za Umma, Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sheria ya Ununuzi, Sheria ya Ukaguzi na kanuni zinazoongoza mzunguko na mchakato wa bajeti nchini.

Rais na Serikali wamepitisha na kuanza kutekeleza mzunguko na mchakato huo mpya wa bajeti bila kujali kwamba suala hilo; pamoja na kanuni za ndani ya Serikali linatawaliwa zaidi na Kanuni za Kudumu za Bunge (Kanuni ya 77 mpaka 82) ambazo hazijafanyiwa marekebisho mpaka sasa.

Tafsiri ya uamuzi huo wa Rais na Serikali wa kuanza kutekeleza mzunguko na mchakato mpya wa bajeti bila kanuni za Bunge kufanyiwa marekebisho ni kwamba Rais na Serikali wanahakika kwamba marekebisho hayo yatafanyika kama serikali ilivyopitisha kwa upande wake; huku ni kulifanya bunge na wabunge kuwa mihuri ya kupitisha tu yaliyopangwa na Serikali (Rubber Stamps).

Rais akiongoza Baraza la Mawaziri wamepitisha na kuanza kutekeleza uamuzi wa kwamba sasa mipango na bajeti ya nchi itajadiliwa na kuidhinishwa na Bunge ya mwisho wa mwaka wa fedha mwishoni mwa mwezi Juni.

Wizara ya Fedha baada ya kupitishwa kwa uamuzi huo imeshaanza kuutekeleza kabla ya marekebisho ya kanuni na tayari imeshatoa miongozo kwa Wizara, Idara na Mamlaka zinazojitegemea, Sekretariati za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuwasilisha makadirio ya bajeti zao mwezi Machi.

Tayari Serikali imeshapanga kwamba Kamati za Kudumu za Kisekta za Bunge zitafanya vikao vya kupitia bajeti mwezi Aprili na hatimaye bajeti za wizara zote kujadiliwa na bajeti ya ujumla kupitishwa ifikapo tarehe 30 Juni 2013; maamuzi hayo yamefanywa na Rais na Baraza la Mawaziri wakati ambapo ratiba za mikutano na vikao vya Bunge hupangwa na Bunge.

Natambua kwamba kwa nyakati mbalimbali wabunge tumetaka marekebisho ya kanuni za Bunge ikiwemo kuhusu mzunguko na mchakato wa bajeti; hata hivyo, Serikali haina madaraka na mamlaka kufanya maamuzi na kuanza kutekeleza mabadiliko hayo bila Bunge kuridhia.

Natoa mwito kwa kila mmoja wetu kutimiza wajibu wa kiraia kudhibiti hali hii kwa kuwa ushiriki wa kibunge kwenye mzunguko na mchakato wa bajeti kuanzia usimamizi wa maandalizi, upitishaji na ufuatiliaji wa utekelezaji ni suala muhimu katika kuhakikisha uwajibikaji kwa maendeleo ya nchi.

Wenu katika uwakilishi wa wananchi,


John Mnyika (Mb)
19/01/2013

Wakurugenzi wa Idara nyeti za serikali Hoi! Dk. Hoseah wa TAKUKURU nje kwa Matibabu, Manumba wa Makosa ya jinai apumulia mashine!


Wakurugenzi wawili wa taasisi nyeti za serikali hivi karibuni wameripotiwa kuwa na matatizo ya kiafya na hali zao kuendelea kutripotiwa kwanza si njema.
Leo gazeti la Mtanzania limeandika kuhusu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) Dk. Joseph Hosea(pichani juu), anaumwa na amepelekwa nje ya nchi kwa matitabu.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya TAKUKURU, Dk. Hosea, alianza kuugua tangu mwanzoni mwa Desemba mwaka jana na ilipofika Desemba 15 hali ilibadilika.

Hata hivyo, chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya TAKUKURU kilisema hadi sasa haijafahamika ugonjwa unaomsumbua.

“Ni kweli Mkurugenzi anaumwa na kuna taarifa yuko ya nje ya nchi kwa matibabu kati ya Ujerumani au Uingereza.

“Kwa mara ya mwisho nilimuona Mkurugenzi akiwa hayupo sawa kiafya na hata alipokuwa anakuja kazini alikuwa katika muonekano ambao ni wazi anaumwa. Lakini katika wiki hizi sijamuona hapa ofisini,” kilisema chanzo hicho cha kuaminika kutoka ndani ya TAKUKURU.

MTANZANIA pia ilimtafuta Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora) George Mkuchika kwa njia ya simu kupata taarifa za kina kuhusu tukio hili lakini alisema hana taarifa yoyote.

“Mhhhh katika hili la ugonjwa wa Dk. Hosea sina taarifa na kama ujuavyo nilikuwa katika msiba wa baba yake Naibu Waziri wa Mifugo, kule Kiteto. Tangu jana nilikuwa n rejea na nimefika Morogoro nimelala hapa na sasa nimeanza safari ya kuelekea Dar es Salaam.

“Kama kuna taarifa yoyote kuhusu hilo kwa sasa siwezi kusema lolote hadi nitakapofika ndugu yangu,” alisema Waziri Mkuchika.

Hata hivyo mmoja wa wafanyakazi wa taasisi hiyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema Dk. Hoseah yupo nje ya nchi kwa mapumziko ya likizo.

“Ni kweli ofisa uhusiano yupo likizo na pia mkubwa (Dk. Hoseah) naye yupo Marekani ameenda kwa ajili ya mapumziko ya likizo hakuna mtu anayeumwa,” alisema.

MTANZANIA ilimtafuta Msemaji wa TAKUKURU Dorine Kapwani ambaye muda wote simu yake ilikuwa ikiita bila kupokewa hata alipopigiwa kwa simu ya mezani.

Mbali na hatua hiyo hata alipotumiwa ujumbe mfupi kwa simu ya kiganjani ambao ulisomeka; “Dada habari, kuna taarifa Dk. Hosea anaumwa na amepelekwa nje ya nchi kwa matibabu je kuna ukweli gani” hakujibu chochote hadi tunakwenda mitamboni jana usiku.

DCI Manumba apumulia mashine

Naye Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba sasa anapumua kwa msaada wa mashine baada ya hali yake kuendelea kuwa mbaya tangu alipofikishwa katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu.

DCI Manumba jana alitumia takribani siku nzima kuwa katika chumba cha uchunguzi kwa ajili ya vipimo zaidi, baada ya kutolewa katika chumba cha uangalizi maalumu (ICU) kwa ajili ya uangalizi wa karibu wa madaktari na wauguzi.

MTANZANIA ilishuhudia DCI akitolewa katika chumba cha wagonjwa mahututi saa 11:25 akipelekwa katika chumba cha uchunguzi huku akiwa amezungukwa na madaktari na wauguzi huku baadhi yao wakiwa wameshikilia vifaa maalumu ambavyo vilikuwa vikimsaidia kupumua.

Hata hivyo, baadhi ya madaktari waliokuwa wamemzunguka hawakuweza kuthibitisha iwapo vifaa alivyokuwa amewekewa DCI Manumba vilikuwa ni sehemu ya mashine iliyokuwa ikimsaidia kupumua.

Hali hiyo iliwafanya ndugu na watoto wa kamanda huyo kuwa katika hali ya taharuki ambako baadhi yao walionyesha kushikwa na huzuni huku mmoja wa watoto wake ambaye jina lake halikupatikana akiwa katika hali ya majonzi makubwa.

Hadi saa 5:45 jioni mgonjwa huyo bado alikuwa hajatolewa katika chumba cha uchunguzi hali iliyowafanya ndugu kuendelea kusubiri katika eneo la mapokezi ya wagonjwa mahututi.

Alihojiwa na waandishi wa habari kuhusu hali ya mgonjwa, Mkurugenzi wa Tiba wa Hospitali hiyo, Dk. Jaffer Dharsee alisema kwa sasa hawezi kusema lolote hadi vipimo vya uchunguzi vitakapokamilika, huku akiwaahidi waandishi wa habari kuwa atatoa taarifa hiyo leo asubuhi.

“Siwezi kusema kitu kwa sasa kwani bado hali ya DCI inahitaji uchunguzi wa karibu wa madaktari na hadi sasa bado yupo katika chumba cha uchunguzi zaidi hivyo sina cha kusema nasubiri nikamilishe ripoti yote labda kesho ndiyo nitakuwa katika nafasi nzuri ya kusema kitu,” alisema Dk Dharsee.

Hata hivyo katika kipindi chote hicho, hali ya ulinzi ilikuwa imeimarika ambako polisi na askari kanzu walikuwa wamezunguka katika maeneo mbalimbali ya hospitali hiyo kuhakikisha kunakuwa na ulinzi wa kutosha.

Viongozi

Jana viongozi mbalimbali waliendelea kufika hospitalini hapo kumjulia hali Manumba. Miongoni mwao ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Silima ambaye aliwasili hospitali hapo mchana pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Meck Sadick.

Viongozi wote hao walipokewa na daktari mkuu wa polisi aliyefahamika kwa jina moja la Dk Makata ambaye aliwapeleka moja kwa moja katika jengo la tatu kilipo chumba cha uchunguzi kwa ajili ya kumjulia hali DCI Manumba.

Dk. Nchimbi baada ya kutoka katika chumba cha mgonjwa hakutaka kuzungumza chochote licha ya kutakiwa kufanya hivyo na waandishi wa habari. “Mnataka niseme nini kwamba mgonjwa hali yake nzuri au mbaya? Mimi si daktari lakini kwa namna nilivyomuona nasema anaendelea vizuri,” alisema Dk. Nchimbi.

DCI Manumba aliugua ghafla na kulazwa katika Hospitali ya Muhimbili na Januari 14 alihamishiwa katika Hospitali ya Aga Khan kwa ajili ya uchunguzi zaidi ambapo alilazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).

Manumba ambaye aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kushika wadhifa huo mwaka 2006 akichukua nafasi ya Adadi Rajabu, haijaelezwa wazi kuwa anasumbuliwa na ugonjwa gani, ingawa taarifa za awali zinasema amekuwa akisumbuliwa na tatizo la figo.

TRA, TUME YA UCHAGUZI NA JUMUIYA YA SERIKALI ZA MITAA (ALAT) WATOA MAONI KATIBA MPYA

Mh. Pinda na Mh. Lowassa wakiwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere jijini Dar


Waziri Mkuu,Mh. Mizengo Pinda akiwa katika mazungumzo na Waziri Mkuu Mstaafu,Mh. Edward Lowasa mara baada yakushuka kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere,jijini Dar es Salaam wakitokea mjini Dodoma.Mh. Pinda alikuwa Dodoma katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Baraza Kuu la wafanyakazi wa Serekali za mitaa.Nyuma yao ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa (TAMISEMI),Mh. Hawa Ghasia akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni,Mh. Jordan Rugimbana ambaye alikuja kumpokea Waziri Mkuu uwanjani hapo.

No comments:

Post a Comment