Saturday, January 19, 2013

Kutoka Kwa Mbunge wa Jimbo la Ubungo-CHADEMA,John Mnyika:'Rais na Mawaziri wanadharau wabunge kuhusu mabadiliko ya mzunguko wa Bajeti.'



 
 Mbunge wa Jimbo la Ubungo-CHADEMA,Mh John Mnyika
---
 
Yaliyojiri na yanayoendelea kujiri ndani ya Baraza la Mawaziri na Wizara ya Fedha kuhusu mabadiliko ya mzunguko na mchakato wa bajeti yanaashiria kwamba Rais na Serikali wanadharau mamlaka na madaraka ya Bunge na wabunge.

Aidha, kutokana na umuhimu wa mzunguko na mchakato wa bajeti katika kuwezesha uwajibikaji kwenye mapato na matumizi ya rasilimali za umma; Waziri wa Fedha anatakiwa aweke wazi kwa umma mabadiliko hayo yaliyofanyika ili wananchi na wadau waweze kutoa maoni na Bunge liweze kuyazingatia wakati wa marekebisho ya kanuni za Bunge yanayotarajiwa kufanywa katika mkutano wa kumi wa Bunge.

Wakati Katibu wa Bunge amenukuliwa tarehe 17 Januari 2013 akisema kwamba pendekezo la mabadiliko ya mzunguko na mchakato wa bajeti bado linajadiliwa na kwamba iwapo litaafikiwa, uamuzi utatangazwa mapema mwezi ujao (Februari 2013) wakati wa mkutano wa Bunge; upande wa Rais na Wizara ya Fedha wameshapitisha na kuanza kutekeleza mzunguko na mchakato mpya wa bajeti kuanzia mwezi Disemba 2012.

Kwa upande wangu nitashiriki vikao vya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Fedha na Uchumi wiki ijayo ili nipate mwanya wa kumhoji Waziri wa Fedha kwa kurejea matakwa ya Katiba ya Nchi, Sheria ya Fedha za Umma, Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sheria ya Ununuzi, Sheria ya Ukaguzi na kanuni zinazoongoza mzunguko na mchakato wa bajeti nchini.

Rais na Serikali wamepitisha na kuanza kutekeleza mzunguko na mchakato huo mpya wa bajeti bila kujali kwamba suala hilo; pamoja na kanuni za ndani ya Serikali linatawaliwa zaidi na Kanuni za Kudumu za Bunge (Kanuni ya 77 mpaka 82) ambazo hazijafanyiwa marekebisho mpaka sasa.

Tafsiri ya uamuzi huo wa Rais na Serikali wa kuanza kutekeleza mzunguko na mchakato mpya wa bajeti bila kanuni za Bunge kufanyiwa marekebisho ni kwamba Rais na Serikali wanahakika kwamba marekebisho hayo yatafanyika kama serikali ilivyopitisha kwa upande wake; huku ni kulifanya bunge na wabunge kuwa mihuri ya kupitisha tu yaliyopangwa na Serikali (Rubber Stamps).

Rais akiongoza Baraza la Mawaziri wamepitisha na kuanza kutekeleza uamuzi wa kwamba sasa mipango na bajeti ya nchi itajadiliwa na kuidhinishwa na Bunge ya mwisho wa mwaka wa fedha mwishoni mwa mwezi Juni.

Wizara ya Fedha baada ya kupitishwa kwa uamuzi huo imeshaanza kuutekeleza kabla ya marekebisho ya kanuni na tayari imeshatoa miongozo kwa Wizara, Idara na Mamlaka zinazojitegemea, Sekretariati za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuwasilisha makadirio ya bajeti zao mwezi Machi.

Tayari Serikali imeshapanga kwamba Kamati za Kudumu za Kisekta za Bunge zitafanya vikao vya kupitia bajeti mwezi Aprili na hatimaye bajeti za wizara zote kujadiliwa na bajeti ya ujumla kupitishwa ifikapo tarehe 30 Juni 2013; maamuzi hayo yamefanywa na Rais na Baraza la Mawaziri wakati ambapo ratiba za mikutano na vikao vya Bunge hupangwa na Bunge.

Natambua kwamba kwa nyakati mbalimbali wabunge tumetaka marekebisho ya kanuni za Bunge ikiwemo kuhusu mzunguko na mchakato wa bajeti; hata hivyo, Serikali haina madaraka na mamlaka kufanya maamuzi na kuanza kutekeleza mabadiliko hayo bila Bunge kuridhia.

Natoa mwito kwa kila mmoja wetu kutimiza wajibu wa kiraia kudhibiti hali hii kwa kuwa ushiriki wa kibunge kwenye mzunguko na mchakato wa bajeti kuanzia usimamizi wa maandalizi, upitishaji na ufuatiliaji wa utekelezaji ni suala muhimu katika kuhakikisha uwajibikaji kwa maendeleo ya nchi.

Wenu katika uwakilishi wa wananchi,


John Mnyika (Mb)
19/01/2013

Wakurugenzi wa Idara nyeti za serikali Hoi! Dk. Hoseah wa TAKUKURU nje kwa Matibabu, Manumba wa Makosa ya jinai apumulia mashine!


Wakurugenzi wawili wa taasisi nyeti za serikali hivi karibuni wameripotiwa kuwa na matatizo ya kiafya na hali zao kuendelea kutripotiwa kwanza si njema.
Leo gazeti la Mtanzania limeandika kuhusu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) Dk. Joseph Hosea(pichani juu), anaumwa na amepelekwa nje ya nchi kwa matitabu.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya TAKUKURU, Dk. Hosea, alianza kuugua tangu mwanzoni mwa Desemba mwaka jana na ilipofika Desemba 15 hali ilibadilika.

Hata hivyo, chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya TAKUKURU kilisema hadi sasa haijafahamika ugonjwa unaomsumbua.

“Ni kweli Mkurugenzi anaumwa na kuna taarifa yuko ya nje ya nchi kwa matibabu kati ya Ujerumani au Uingereza.

“Kwa mara ya mwisho nilimuona Mkurugenzi akiwa hayupo sawa kiafya na hata alipokuwa anakuja kazini alikuwa katika muonekano ambao ni wazi anaumwa. Lakini katika wiki hizi sijamuona hapa ofisini,” kilisema chanzo hicho cha kuaminika kutoka ndani ya TAKUKURU.

MTANZANIA pia ilimtafuta Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora) George Mkuchika kwa njia ya simu kupata taarifa za kina kuhusu tukio hili lakini alisema hana taarifa yoyote.

“Mhhhh katika hili la ugonjwa wa Dk. Hosea sina taarifa na kama ujuavyo nilikuwa katika msiba wa baba yake Naibu Waziri wa Mifugo, kule Kiteto. Tangu jana nilikuwa n rejea na nimefika Morogoro nimelala hapa na sasa nimeanza safari ya kuelekea Dar es Salaam.

“Kama kuna taarifa yoyote kuhusu hilo kwa sasa siwezi kusema lolote hadi nitakapofika ndugu yangu,” alisema Waziri Mkuchika.

Hata hivyo mmoja wa wafanyakazi wa taasisi hiyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema Dk. Hoseah yupo nje ya nchi kwa mapumziko ya likizo.

“Ni kweli ofisa uhusiano yupo likizo na pia mkubwa (Dk. Hoseah) naye yupo Marekani ameenda kwa ajili ya mapumziko ya likizo hakuna mtu anayeumwa,” alisema.

MTANZANIA ilimtafuta Msemaji wa TAKUKURU Dorine Kapwani ambaye muda wote simu yake ilikuwa ikiita bila kupokewa hata alipopigiwa kwa simu ya mezani.

Mbali na hatua hiyo hata alipotumiwa ujumbe mfupi kwa simu ya kiganjani ambao ulisomeka; “Dada habari, kuna taarifa Dk. Hosea anaumwa na amepelekwa nje ya nchi kwa matibabu je kuna ukweli gani” hakujibu chochote hadi tunakwenda mitamboni jana usiku.

DCI Manumba apumulia mashine

Naye Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba sasa anapumua kwa msaada wa mashine baada ya hali yake kuendelea kuwa mbaya tangu alipofikishwa katika Hospitali ya Aga Khan, Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu.

DCI Manumba jana alitumia takribani siku nzima kuwa katika chumba cha uchunguzi kwa ajili ya vipimo zaidi, baada ya kutolewa katika chumba cha uangalizi maalumu (ICU) kwa ajili ya uangalizi wa karibu wa madaktari na wauguzi.

MTANZANIA ilishuhudia DCI akitolewa katika chumba cha wagonjwa mahututi saa 11:25 akipelekwa katika chumba cha uchunguzi huku akiwa amezungukwa na madaktari na wauguzi huku baadhi yao wakiwa wameshikilia vifaa maalumu ambavyo vilikuwa vikimsaidia kupumua.

Hata hivyo, baadhi ya madaktari waliokuwa wamemzunguka hawakuweza kuthibitisha iwapo vifaa alivyokuwa amewekewa DCI Manumba vilikuwa ni sehemu ya mashine iliyokuwa ikimsaidia kupumua.

Hali hiyo iliwafanya ndugu na watoto wa kamanda huyo kuwa katika hali ya taharuki ambako baadhi yao walionyesha kushikwa na huzuni huku mmoja wa watoto wake ambaye jina lake halikupatikana akiwa katika hali ya majonzi makubwa.

Hadi saa 5:45 jioni mgonjwa huyo bado alikuwa hajatolewa katika chumba cha uchunguzi hali iliyowafanya ndugu kuendelea kusubiri katika eneo la mapokezi ya wagonjwa mahututi.

Alihojiwa na waandishi wa habari kuhusu hali ya mgonjwa, Mkurugenzi wa Tiba wa Hospitali hiyo, Dk. Jaffer Dharsee alisema kwa sasa hawezi kusema lolote hadi vipimo vya uchunguzi vitakapokamilika, huku akiwaahidi waandishi wa habari kuwa atatoa taarifa hiyo leo asubuhi.

“Siwezi kusema kitu kwa sasa kwani bado hali ya DCI inahitaji uchunguzi wa karibu wa madaktari na hadi sasa bado yupo katika chumba cha uchunguzi zaidi hivyo sina cha kusema nasubiri nikamilishe ripoti yote labda kesho ndiyo nitakuwa katika nafasi nzuri ya kusema kitu,” alisema Dk Dharsee.

Hata hivyo katika kipindi chote hicho, hali ya ulinzi ilikuwa imeimarika ambako polisi na askari kanzu walikuwa wamezunguka katika maeneo mbalimbali ya hospitali hiyo kuhakikisha kunakuwa na ulinzi wa kutosha.

Viongozi

Jana viongozi mbalimbali waliendelea kufika hospitalini hapo kumjulia hali Manumba. Miongoni mwao ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Silima ambaye aliwasili hospitali hapo mchana pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Meck Sadick.

Viongozi wote hao walipokewa na daktari mkuu wa polisi aliyefahamika kwa jina moja la Dk Makata ambaye aliwapeleka moja kwa moja katika jengo la tatu kilipo chumba cha uchunguzi kwa ajili ya kumjulia hali DCI Manumba.

Dk. Nchimbi baada ya kutoka katika chumba cha mgonjwa hakutaka kuzungumza chochote licha ya kutakiwa kufanya hivyo na waandishi wa habari. “Mnataka niseme nini kwamba mgonjwa hali yake nzuri au mbaya? Mimi si daktari lakini kwa namna nilivyomuona nasema anaendelea vizuri,” alisema Dk. Nchimbi.

DCI Manumba aliugua ghafla na kulazwa katika Hospitali ya Muhimbili na Januari 14 alihamishiwa katika Hospitali ya Aga Khan kwa ajili ya uchunguzi zaidi ambapo alilazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).

Manumba ambaye aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete kushika wadhifa huo mwaka 2006 akichukua nafasi ya Adadi Rajabu, haijaelezwa wazi kuwa anasumbuliwa na ugonjwa gani, ingawa taarifa za awali zinasema amekuwa akisumbuliwa na tatizo la figo.

TRA, TUME YA UCHAGUZI NA JUMUIYA YA SERIKALI ZA MITAA (ALAT) WATOA MAONI KATIBA MPYA

Mh. Pinda na Mh. Lowassa wakiwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere jijini Dar


Waziri Mkuu,Mh. Mizengo Pinda akiwa katika mazungumzo na Waziri Mkuu Mstaafu,Mh. Edward Lowasa mara baada yakushuka kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere,jijini Dar es Salaam wakitokea mjini Dodoma.Mh. Pinda alikuwa Dodoma katika ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa Baraza Kuu la wafanyakazi wa Serekali za mitaa.Nyuma yao ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa (TAMISEMI),Mh. Hawa Ghasia akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni,Mh. Jordan Rugimbana ambaye alikuja kumpokea Waziri Mkuu uwanjani hapo.

Monday, January 14, 2013

MAKAMU WA RAIS DKT. BILAL AENDESHA KIKAO CHA MUUNGANO MJINI ZANZIBAR LEO


 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiendesha Kikao cha Muungano, kilichofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Beach Resort, mjini Zanzibar leo, Januari 14, 2013. Wa pili (kushoto) ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda (wa pili (kulia) Ni Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd (kushoto) ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samiah Suluhu na (kulia) ni Waziri wa nchi Ofsi ya Makamu wa pili wa Rais zanzibar, Mohamed Aboud. 
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiteta jambo na Makamu wa pili wa Rais, Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, wakati Makamu alipokuwa akiendesha Kikao cha Muungano kilichofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Beach Resort, mjini Zanzibar leo.
 Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Sazi Salula (kulia) Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Eng. Ngosi Mwihava (katikati) na Mkurugenzi wa Muungano, Rajab Baraka (kushoto) wakifuatilia vifungu katika machapisho ya kujadili masuala ya Muungano, wakati wa kikao cha Muungano, kilichoendeshwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal (hayupo pichani), kilichofanyika leo Januari 14, 2013, katika ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Beach Resort, mjini Zanzibar. 
 Baadhi ya Mawaziri wakiwa ukumbini humo wakati wakifuatilia kikao hicho cha Muumgano kilichoendeshwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, (hayupo pichani), leo katika Ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Beach Resort, mjini Zanzibar.
 Baadhi ya Mawaziri wakiwa ukumbini humo wakati wakifuatilia kikao hicho cha Muumgano kilichoendeshwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, (hayupo pichani), leo katika Ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Beach Resort, mjini Zanzibar.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiagana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Samiah Suluhu, mara baada ya kumalizika kwa kikao cha Muungano, kilichofanyika leo Januari 14, 2013 katika Ukumbi wa Hoteli ya Zanzibar Beach Resort, mjini Zanzibar.

WANAFUNZI IFM WAVAMIA WIZARA YA MAMBO YA NDANI NI BAADA YA KUKOSA ULINZI KWENYE HOSTELI, BAADA YA WENZAO WAKIUME WAWILI KUBAKWA NA MAJAMBAZI NA KULAZWA HOSPITALI. SAKATA LINAENDELEA KIGAMBONI MIDA HII CHINI YA USIMAMIZI WA KAMANDA KOVA


Wanafunzi wa Chuop Cha Uongozi wa Fedha cha jijini Dar es Salaam (IFM) wakiwa mbele ya geti la Wizara ya Mambo ya ndani walipovamia leo majira ya saa nne na nusu asubuhi wakiwa na madai ya kutopewa ulinzi na jeshi la polisi kwenye makazi yao ya Hosteli za Kigamboni kutokana na kuvamiwa na majambazi mara kwa mara. Wanafunzi hao walidai siku ya Ijumaa walifanya kikao na jeshi hilo ili wawape ulinzi lakini suala la ajabu siku waliyofanya kikao na Jeshi hilo ndio siku waliovamiwa wenzao wawili wakiume na kubakwa  hali iliyosababishwa wanafunzi hao kubakwa. Majambazi hao wamekua wakidai kupewa Laptop simu na fedha kama mwanafunzi akikataa humfanyia vitendo vya kulawiti.
Ulinzi uliimarishwa nje ya jengo la Wizara ya Mambo ya ndani kufuatia kadhia hiyo ya wanafunzi.
Kamanda wa Polisi wa Kanda maalum ya Kipolisi ya jiji la Dar es Salaam Suleiman Kova akimsikiliza Rais wa Serikali ya wanafunzi ya Chuo cha IFM mara baada ya kuwasili eneo la ofisi za Wizara ya Mambo ya ndani ambapo aliwaamuru wanafunzi hao wafuatane waende hadi Kigamboni kwenye Kituo walichoripoti taarifa zao pamoja na kwenda kwenye Hosteli zao. Kova aliahidi kushughulikia jambo hilo kwa haraka bila kusita.
"Wanafunzi wenzetu wa kiume wamelawitiwa nyinyi tumewapa taarifa siku ya ijumaa kuwa hatunaulinzi tunaibiwa hovyo vitu vyetu halafu siku hiyo hiyo unafanyika ubakaji huo"
Baadhi ya wanafunzi wakiwa kwenye mitaa ya Posta jijini humo wakielekea kwenye kivuko cha Kigamboni ili kwenda kumuonyesha Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Kipolisi ya jiji la Dar es Salaam Suleiman Kova.
Wakianza maandamano kuelekea Feli kwaajili ya kuvuka kwenda Kigamboni.
Kova akitoa maelezo kwa waandishi wa habari juu ya hatua zitakazochukuuliwa baada ya kupata taarifa hizo ambapo aliwaamuru wanafunzi hao wote kwapamoja kwenda Kigamboni kufuatilia tukio hilo kwa pamoja.
Mitaani Posta.
Hadi kieleweke!
Tunaimba! Tunavuka bure Tunavuka bure kwenye Pantoni.
Kova akishangiliwa wakati wa safari kuelekea Feli.
Kwenye Kona ya feli kuwania geti ili waingie bure!
Wakajazana kupita kiasdi Kova akazuia kivuko kisiondoke hadi wapungue!
Hapa wakigoma kupungua kazi iliyochukua zaidi ya Saa moja hadi kivuko kuendelea na kazi ya kuvusha abiria
Pamoja na kutakiwa kupungua hapa wengine walizidi kuendelea kuingia na kukijaza kivuko hicho. Picha zote na Raha za Pwani, hii ni sehemu ya kwanza tutawaletea sehemu ya pili ya tukio hili ambalo hadi hivi sasa filamu inaendelea hapa feli na ikielekea Kigamboni.Picha Kwa Hisani Ya Mtaa Kwa Mtaa Blog

mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya bia ya serengeti steve gannon atembelea mjengoni clouds media group.



Mkurugenzi Mtendaji wa Clouds Media Group,Joseph Kusaga 'Joe' pichani kushoto akichanganua jambo kwa Mkurungezi Mtendaji wa Kampuni ya bia ya Serengeti,Steve Gannon mara baada ya kutembezwa studio mpya na ya kisasa kabisa,iliyofungwa mjengoni humo,ambayo inatarajia kuanza kutumika hivi karibuni,Steve Gannon amefanya ziara fupi mwishoni mwa wiki na kutembelea vitengo vyote kampuni hiyo huku akijionea namna shughuli mbalimbali zinavyofanyika mjengoni humo.
Steve Gannon akitazama picha za wasanii mbalimbali wa nje waliowahi kufika nchini Tanzania na kufanya maonesho yao kadhaa ndani ya ofisi za Prime Time Promotions Ltd.


Mkurugenzi wa mambo ya utafiti na vipindi vya Clouds Media Group,Ruge Mutahaba akifafanua jambo kwa Mkurungezi Mtendaji wa Kampuni ya bia ya Serengeti,Steve Gannon ambaye nae alikuwa akimsikiliza kwa makini.
Mkurungezi Mtendaji wa Kampuni ya bia ya Serengeti,Steve Gannon akimuuliza jambo mtangazaji wa kipindi cha Power Breakfast,Gerald Hando kuhusiana na mambo mbalimbali ya kikazi,alipotembezwa kwenye studio ya ziada.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Clouds Media Group,Joseph Kusaga 'Joe' pichani kushoto akifafanua jambo kwa Mkurungezi Mtendaji wa Kampuni ya bia ya Serengeti,Steve Gannon mara baada ya kufanya ziara fupi mwishoni mwa wiki na kutembelea vitengo vyote kampuni hiyo huku akijionea namna shughuli mbalimbali zikifanya mjengoni humo.

Mkurungezi Mtendaji wa Kampuni ya bia ya Serengeti,Steve Gannon akizungumza jambo na baadhi ya wafanyakazi wa kitengo muhimu cha kampuni hiyo cha Masoko.
Steve Gannon akisalimiana na Oparesheni Meneja wa Prime Time Promotions Ltd.Balozi Kindamba,mara alipotembelea ndani ya kampuni hiyo ambayo imekuwa ikijihusisha na matamasha mbalimbali likiwemo tamasha kubwa la Fiesta ambalo hufanyika kila mwaka.
Steve Gannon akisalimiana na Gerald Hando
Mkurungezi Mtendaji wa Kampuni ya bia ya Serengeti,Steve Gannon akioneshwa matoleo mbalimbali ya jariba la burudani la KITANGOMA linachapishwa na kampuni ya Prime Time Promotions.


Mkurungezi Mtendaji wa Kampuni ya bia ya Serengeti,Steve Gannon akipeana mkono na Mmoja wa wafanyakazi wa Prime Time Promotions,Godliva Nicholaus mara alipowasili ndani ya ofisi za kampuni hiyo.
Mkurugenzi wa mambo ya Masoko na Mauzo,Shebba Kusaga akifafanua jambo kwa Mkurungezi Mtendaji wa Kampuni ya bia ya Serengeti,Steve Gannon.
Chief Editor wa Clouds TV,Bwa.Kanyopa akitoa maelezo mafupi kuhusiana na ufanyaji wao kazi ikiwemo na urushaji wa vipi kupitia Tv yao,Pichani kushoto ni Boss Joe akisikiliza kwa makini.


Mkurungezi Mtendaji wa Kampuni ya bia ya Serengeti,Steve Gannon alitembezwa pia ndani ya chumba maalum cha kuandalia habari,hapa Mtangazaji wa kipindi cha Michezo Shaffih Dauda akifafanua jambo kwa Steve Gannon.
Baada ya ziara kutembelea vitengo mbalimbali vya kampuni hiyo,pia Steve Gannon alipata wasaa wa kukaa meza moja na uongozi wa juu wa kampuni hiyo na kuzungumza machache,ikiwa ni sehemu ya mchakato wa ufanisi wa kikazi kwa mwaka mpya wa 2013. 

ALAMA YA BARABARANI HAIELEWEKI AU NDIO MAKUSUDI

Malori yakiwa yameegeshwa ndani ya hifadhi ya barabara ya mandela karibu na kituo Cha Gereji Huku kibao Cha Alama za Barabarani ambcho kinaonyesha alama ya kutokurusu Kuegesha Kikiwa Pembeni ya malori hayo. Je hii ni dharau au mwenye malori hayo yupo Juu ya Sheria au yupo sahihi kwa kuegesha magari yake hapo?

BALOZI WA NIGERIA NCHINI MAREKANI AMFANYIA DINNER YA KUMUAGA BALOZI WETU MH. MWANAID MAAJAR


Balozi wa Tanzania nchini Marekani na Mexico Mhe. Mwanaidi Maajar (wapili toka kulia)akiingia nyumbani kwa Balozi wa Nigeria (hayupo pichani) Potomac, Maryland, huku wakipokelewa na afisa ubalozi wa Nigeria (wa kwanza kulia) anayesalimia ni mama Lily Munanka ambaye ni mkuu wa utawala na fedha Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani akifuatiwa na mume wa Balozi, Bwn. Shariff Maajar siku ya Jumapili January 6, 2013 siku Balozi wa Nigeria alipomfanyia chakula cha jioni maalum kwa ajili ya kumuaga Balozi wetu ambaye anamaliza muda wake.
Mhe. Mwanaidi Maajar akilakiwa na Balozi wa Nigeria nchini Marekani, Mhe.Adebowale Ibidpo Adefuye siku ya Jumapili January 6, 2013 alipomkaribisha chakula cha jioni maalum kwa ajili ya kumuaga Balozi wa Tanzania nchini Marekani ambaye anamaliza muda wake.
Mke wa Balozi wa Nigeria akisalimiana na kumkaribisha Mhe. Mwanaidi Maajar huku mumewe Bwn. Shariff Maajar akiwa amesimama kwenye ngazi akiangalia.
Balozi na mumewe Bwn. Shariff Maajar wakisalimiana na Rais wa Jumuiya ya Watanzania DMV, Bwn Idd Sandaly ambaye pia aliongozana na mkewe (wakwanza kushoto) kwenye chakula cha jioni alichoandaliwa Balozi wetu na Balozi wa Nigeria kwa ajili ya kumuaga siku ya Jumapili January 6, 2013 nyumbani kwake Potomac, Maryland.
Kutoka kushoo ni Rais wa Jumuiya ya Watanzania DMV akiwa pamoja na mkewe, Balozi wa Benin nchini Marekani Mhe.Cyrille S. Oguin katika picha ya pamoja na Balozi wa Nigeria nchini Marekani Mhe.Adebowale Ibidpo Adefuye.
Balozi wa Nigeria nchini Marekani Mhe.Adebowale Ibidpo Adefuye (kulia) akisalimiana na Mume wa Balozi wa Tanzania nchini Marekani na Mexico, Bwn. Shariff Maajar.
Balozi wa Nigeria nchini Marekani Mhe.Adebowale Ibidpo Adefuye akisalimiana na kumkaribisha Balozi wa Botswana nchini Marekani Mhe. Tebelelo Seretse nyumbani kwake Potomac, Maryland siku ya Jumapili January 6, 2013 alipomualika chakula cha jioni maalum kwa ajili ya kumuaga Balozi wetu ambaye anamaliza muda wake.
Balozi wa Botswana nchini Marekani Mhe. Tebelelo Seretse (kushoto) akiongea jambo na Balozi wa Tanzania nchini Marekani na Mexico, Mhe. Mwanaidi Maajar.
Kutoka kushoto ni Mkuu wa Utawala na Fedha Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani na Mexico, mama Lily Munanka, Mke wa Balozi wa Zimbabwe, Balozi wa Zimbabwe nchini Marekani, Mhe. Dr. Machivenyika Mapuranga na Balozi wa Benin nchini Marekani Mhe. Cyrille S. Oguin.
Wakati wa chakula.Picha na Vijimambo Blog