Friday, December 28, 2012

POLISI WAKAMATWA KWA KUUA MWANAKIJIJI KIGOMA


Kamanda Fraiser Kashai.
Jeshi la Polisi  mkoani Kigoma linawashikilia askari wake wawili kwa tuhuma za kumpiga na kusababisha kifo cha mkazi wa kijiji cha Herushingo, wilayani Kasulu, mkoani Kigoma, Gasper Mussa.

Kamanda wa Polisi mkoani Kigoma, Fraiser Kashai, aliwataja askari hao kwa waandishi wa habari mjini hapa kuwa ni mwenye namba NCC 8622 Koplo Peter na G.1236 Konstebo Sunday. Alisema wawili hao wanadaiwa kumpiga Mussa walipokuwa kwenye kilabu cha pombe usiku wa Sikukuu ya Krismasi.

Kwa mujibu wa maelezo ya Kamanda Kashai, Mussa alifariki siku moja baada ya kupata kipigo hicho alipokuwa akipelekwa hospitalini baada ya kukaa mahabusu kwa siku moja.

Akisimulia tukio hilo, Kamanda Kashai alisema siku ya tukio, Mussa na askari hao walikuwa wakinywa pombe katika kilabu cha pombe na wakati wakinywa, ikatokea vurugu ambapo inadaiwa kusababishwa na Mussa kukataa kulipa pombe aliyokunywa.

Baada ya Mussa kukataa kulipa, Kamanda Kashai alisema askari hao ambao kwa sasa wanahifadhiwa katika Kituo Kikuu cha Polisi wilayani Kasulu, walianza kumuadhibu kwa kumpiga na baadaye walienda kumlaza mahabusu. 

Hata hivyo, siku iliyofuata, Kamanda Kashai alisema Mussa alizidiwa ndipo Mkuu wa Kituo cha Polisi Herushingo, alianza jitihada za kumpeleka Mussa hospitali, lakini alifariki mikononi mwa polisi kabla ya kufikishwa hospitali.
Alisema baada ya tukio hilo, alituma askari wake kufuatilia kwa undani kujua kile kilichotokea ili wachukue hatua.

Kwa sasa Kamanda Kashai alisema hatua za kijeshi kwa askari hao zinaendelea  ikiwa ni pamoja na kuwavua hadhi ya kijeshi waliyonayo kabla ya kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

Katika tukio lingine Polisi mkoani Kigoma inamshikilia Hassan  Shija, mwalimu wa fani ya umeme katika Chuo cha Mamlaka ya Elimu na Ufundi Stadi (Veta) mkoani Kigoma kwa tuhuma za kumpiga mapanga na kumjeruhi mke wake sehemu mbalimbali za mwili wake.

Kamanda Kashai alimtaja mwanamke huyo kuwa ni Rida Mbili ambaye amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Kigoma ya Maweni na kwamba chanzo cha mgogoro huo ni wivu wa mapenzi.
 
Chanzo : Zero 99

Naibu Waziri Wa Habari Aongea Na Wadau Wa Filamu Nchini

 Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mheshimiwa Amos Makala akiongea na wadau wa tasnia ya filamu kuhusu urasimishaji wa tasnia ya filamu nchini.Picha Na Benjamin Sawe

MAKACHERO KUTOKA DAR WATUA ZANZIBAR KUCHUNGUZA SHAMBULIO LA PAROKO


Na Mohammed Mhina, wa Jeshi la Polisi Zanzibar

Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Dar es Salaam, imetuma timu ya Makachero kuja Zanzibar kuungana na wenzao wengine wa Polisi Zanzibar katika Upelelezi wa tukio la kushambuliwa kwa Paroko wa Parokia ya Mpendae Amrose Nkenda (pichani).

Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa makosa ya Jinai Zanzibar ACP Yusuf Ilembo, amesema kuwa timu hiyo ambayo inaongozwa na Afisa mmoja wa ngazi ya juu (hakumtaja jina) ina jumla ya Makachero watano waliobobea katika masuala ya upelelezi hapa nchini.

Amesema kuwa nia ya Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali Saidi Mwema, kuituma timu hiyo kuja hapa Zanzibar, ni kutaka kuengeza nguvu katika tukio hili ambalo linatazamwa kwa aina tofauti hasa ikizingatiwa kuwa aliyeshambuliwa ni Kiongozi mkubwa wa dini na limetokea katika kipindi cha siku kuu ya Krismas.

Amesema Jeshi la Polisi limeamua tukio hili kupelelezwa kwa pamoja kati ya wenzao wa makao makuu ya Polisi Dar es salaam na wa hapa Zanzibar ili kuhakikisha kuwa wale wote waliohusika katika kumshambulia Paroko huyo wanakamatwa.

Hata hivyo kamanda Ilembo amesema kuwabado Polisi wanaendelea na Upelelezi wa kubaini sababu za kushambuliwa kwa Paroko huyo bila ya kuibwa kwa kitu chochote kutoka kwa mshambuliwa.

Amesema kuna uwezekana kuwa watuhumiwa wameshindwa kuchukua kitu chochote baada ya kubaini kuwa eneo la tukio lisingekuwa salama kwao kwa vile kulikuwa na walinzi na ni eneo ambalo ni karibu kabisa na makazi ya viongozi wengine wa dhehebu hilo.

Akizungumzia siku kuu ya mwisho wa mwaka 2012 na mwanzoni mwa mwaka 2013, Kamanda Ilembo amewahimiza wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa pale wanapobaini kuwepo kwa wahalifu ili wachukuliwe hatua.

Naye Kamanda wa Polisi mkoa wa Mjini Magharibi Zanzibar ACP Aziz Juma Mohammed, amewatahadharisha wazazi na walezi kutowaruhusu watoto wadogo kuranda barabarani ama kwenda katika fukwe za bahari kuogelea pasipo uangalizi wa watu wazima.

Kamanda Aziz amesema kuwa uzoefu unaonyesha kuwa watoto wengi wamekuwa wakigongwa na magari ama kuzama na kufa maji katika siku hizi za siku kuu za mwisho wa mwaka kwa kukosa uwangalizi wa watu wazima.

Aidha amewataka wananchi kutoziacha nyumba zao wazi ama bila ya kuwa na uwangalizi wa kutosha ili kutowapa nafasi kwa wahalifu kupata fursa ya kuwaiba.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Atembelea Makazi ya padri Ambrose Mkenda Paroko wa kanisa katoliki la Mpendae Zanzibar na kuupa pole uongozi wa Kanisa hilo pamoja na Familia yake kufwatia ajali ya kupigwa risasi hivi karibuni na watu wasioujulikana

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiangalia gari ya Paroko wa Parokia ya Mpendae Padre Ambrose Mkenda ambayo alikuwa akiendesha na kuvamiwa kwa risasi ya watu wasiojuilikana
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akipata maelezo kutoka kwa Uongozi wa Skuli ya Francis Maria Tomondo ambapo Padre Ambrose Mkenda wa Paroko ya Parokia ya Mpendae alijeruhiwa kwa risasi hivi karibuni
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akifuatana na Father Shayo wa Kanisa la Roman Catholic liliopo minara miwili baada kuwafariji na kutoa mkono wa pole kwa uongozi wa huo kufuatia kujeruhiwa kwa Paroko wa Parokia ya Mpendae Padre Ambrose Mkenda.
---
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alifika katika makazi ya padri Ambrose Mkenda wa Paroko wa parokia ya kanisa katoliki la Mpendae Zanzibar kuupa pole uongozi wa Kanisa hilo pamoja na Familia yake kufuatia ajali ya kupigwa risasi hivi karibuni na watu wasioujulikana. 
Tukio hilo la kusikitisha lililofanywa na watu wawili waliopakiana kwenye Vespa lilitokea langoni mwa Skuli ya Francis Maria iliyopo Tomondo Wilaya ya Magharibi ambapo ndio makaazi ya Padri Ambrose.

Balozi Seif akiufariji Uongozi huo alisema ni jambo baya na la kusikitisha lililofanywa na watu hao ambalo limetoa sura mbaya kwa Taifa na Serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi itaendelea kufanya uchunguzi wa tukio hilo na haitasita kuwachukuliwa hatua za kisheria watu watakaobainika kufanya uhalifu huo.
Alisema Serikali imesikitishwa na kulaani kitendo cha watu hao ambacho kinaashiria uvunjifu wa amani pamoja na kuwaweka wananachi katika hali ya wasi wasi usio wa lazima ndani ya harakati zao za kimaisha. 
Akitoa shukrani kwa niaba ya Uongozi na Familia ya Padre Ambrose Mkenda Kiongozi kutoka Kanisa la Roman Catholic Father Shayo aliiomba Serikali kuendelea kuimarisha ulinzi wa raia wema ili kupunguza hofu iliyotanda mioyoni mwao kutokana na matukio ya uvamizi.
Father Shayo alitahadharisha kwamba hulka mbaya iliyoanzishwa na baadhi ya watu kuwafundisha watoto wadogo tabia ya kukashifu watu wazima kwa sababu ya utofauti wa Kidini inawajengea maisha mabovu watoto hao. “ Watoto wadogo kufundishwa tabia ya kukashifu watu wengine tuelewe kwamba Taifa halitakuwa na muelekeo mwema wa jamii yake ya baadaye”. Alitahadharisha Father Shayo. 
  Na 
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar

Kipanya LEO

Naibu katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Eng. Ngosi Mwihava Afungua Warsha kwa maafisa wa mipakani kuhusu usimamizi wa mazao na bidhaa zitokanazo na Bioteknolojia ya kisasa

 Naibu katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Eng. Ngosi Mwihava akifungua Warsha kwa maafisa wa mipakani kuhusu usimamizi wa mazao na bidhaa zitokanazo na Bioteknolojia ya kisasa. Kulia ni Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Dkt. Julius Ningu na kushoto ni Afisa Mazingira Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi Esta Makwaia. Warsha hii imefanyika leo kwenye Hotel ya La kairo jijini Mwanza
 Baadhi ya Washiriki wa Warsha ya Usimamizi wa mazao na bidhaa zitokanazo na bioteknolojia ya kisasa wakimsikiliza Mgeni Rasmi Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Eng. Ngosi Mwihava [pichani hayupo] kwenje Hoteli ya La kairo Jiji Mwanza
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Eng. Ngosi Mwihava akisalimiana na Afisa Afya Mkoa wa Shinyanga Bw. Nyanza Masakilija mara Baada ya Ufunguzi wa Warsha ya Usimamizi wa Mazao na bidhaa zitokanazo na Bioteknolojia ya kisasa katika Hoteli ya La Kairo Jiji Mwanza
Washiriki wa Warsha ya Usimamizi wa mazao na bidhaa zitokanazo na bioteknolojia ya kisasa wakiwa kwenye picha ya pamoja na mgeni rasmi (katikati) Mara baada ya kufungua warsha hiyo kwenye Hoteli ya La kairo Jiji Mwanza.Picha na Ali Meja

TAARIFA KUTOKA KWA MBUNGE WA JIMBO LA UBUNGO, JOHN MNYIKA

Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika (Mb)

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Nakusudia kutumia kifungu cha 10 cha Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge kutaka nakala ya mkataba wa mkopo wa masharti kiasi cha Dola za Marekani bilioni 1.225 (shilingi trilioni 1.86) kutoka China.

Nitataka pia nakala za mikataba wa mradi wa miundombinu ya gesi asilia ambayo itahusisha ujenzi wa mitambo ya kusafishia gesi asilia katika mikoa ya Lindi na Mtwara na ujenzi wa bomba kuu la kusafirishia gesi asilia la inchi 36 kutoka Mtwara kupitia Lindi, Pwani hadi Dar es Salaam lenye umbali wa kilometa 532.

Hii ni kwa sababu mpaka sasa Wizara ya Nishati na Madini haijatekeleza pendekezo nililowasilisha bungeni tarehe 27 Julai 2012 kwamba kutokana na unyeti wa mradi huo kwa mustakabali wa nchi na maisha ya wananchi wa sasa na baadaye Serikali ilipaswa kuwasilisha bungeni na kuweka wazi kwa umma mkataba wa mradi husika.

Pendekezo hilo lingeliwezesha Bunge kuishauri na kuisimamia serikali kuanzia katika hatua za awali kuhakikisha kwamba maslahi ya taifa yanalindwa katika hatua zote na pia wananchi wananufaika kutokana na fursa za uwekezaji huo mkubwa.
Kutokana na Serikali kutokuzingatia pendekezo hilo na badala yake Rais Jakaya Kikwete kufanya uzinduzi wa mradi huo tarehe 8 Novemba 2012 Mkoani Dar es salaam huku usiri ukiendelezwa malalamiko yameanza kujitokeza katika maeneo ya mradi husika hususan katika Mkoa wa Mtwara.

Aidha, Serikali irejee katika mapendekezo niliyotoa bungeni na kutoa maelezo kwa umma ya sababu za bomba hilo kujengwa kutoka Mtwara mpaka Dar es salaam na kueleza kwa uwazi manufaa ya mradi huo na miradi mingine inayopaswa kutekelezwa katika mikoa ya Kusini kwa maendeleo ya wananchi husika.

Tarehe 27 Julai 2012 nilieleza bungeni kuwa pamoja na ujenzi wa mitambo miwili ya kusafishia gesi asili Mnazi Bay na Songo Songo kama sehemu ya mradi huo; Serikali inapaswa kueleza ni miradi ipi inayoambatana na mradi huo ambayo imepangwa kuwanufaisha wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara ikiwemo kuharakisha utekelezaji wa mradi wa kuzalisha umeme wa MW 300 Mtwara na MW 230 wa Somanga Fungu (Kilwa).

Kwa upande mwingine, utekelezaji wa mradi huo unaendelea bila kuwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ambayo ingepaswa kuishauri na kuisimamia Serikali hivyo ni muhimu Spika wa Bunge akachukua hatua kutokana na barua niliyomwandikia mwanzoni mwa mwezi Oktoba 2012 ambayo mpaka sasa haijajibiwa.

Ikumbukwe kwamba katika barua hiyo nilitoa mwito kwa Spika atumie madaraka na mamlaka yake kutangaza kwa umma kamati nyingine ya kudumu ya Bunge itayoshughulikia nishati na madini ikiwemo masuala ya gesi asili kwa sasa kufuatia hali tete na tata kuhusu sekta ndogo ya gesi asilia nchini na kwa kuzingatia umuhimu na unyeti wa sekta hiyo katika uchumi wa nchi na maisha ya wananchi.

Pamoja na mambo mengine nilipendekeza Spika aelekeze kamati hiyo kupokea na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge ya mwaka 2011 kuhusu Sekta Ndogo ya Gesi Asili ikiwemo juu ya hatua iliyofikiwa katika kushughulikia tuhuma za ufisadi, madai ya mapunjo ya fedha za mauzo ya Gesi asili na hatua iliyofikiwa katika maandalizi ya sera, mpango mkakati na sheria ya gesi asili.

Hatua hii ni muhimu kwa sasa kwa kuwa hata baada ya uamuzi wake kuhusu tuhuma za rushwa kwa wajumbe wa Kamati husika, Spika hakueleza hatma ya Kamati ya Nishati na Madini iliyovunjwa hali ambayo imeacha ombwe la uongozi na usimamizi wa kibunge (Parliamentary Oversight) kwenye sekta hizi nyeti kwa uchumi wa nchi na maisha ya wananchi.

John Mnyika (Mb) Waziri Kivuli wa Nishati na Madini 26/12/2012

GESI CHANZO CHA MATATIZO KWA NCHI ZA WENZETU , JE TANZANIA ITAPONA KWA HILI?

Pichani Juu Ni Mabango yaliyokuwa yamebebwa Jana na Wakazi wa Mtwara wakati wa Maandamano ya Kupinga Ujenzi wa Bomba la Gesi
................................................................................

MAELFU ya wakazi wa Mkoa wa Mtwara jana waliandamana wakipinga uamuzi wa Serikali kusafirisha gesi kwa njia ya bomba kutoka hapa kwenda Dar es Salaam.

Maandamano hayo ambayo yaliwashirikisha wananchi wa wilaya za mkoa huu zikiwamo Tandahimba na Newala, yalianzia katika Kijiji cha Mtawanya hadi Mtwara mjini kupitia barabara ya kwenda Msimbati eneo ambako gesi asilia inapatikana.

Waandamanaji hao waliotembea umbali wa kilomita sita, walitoa maazimio tisa mojawapo likihoji sababu za mitambo ya kuzalisha umeme kutojengwa Mtwara ambako ni jirani na inakochimbwa gesi hiyo.

Katika tamko hilo lenye kurasa mbili, waandamanaji hao wamesema Serikali haijaweka wazi namna gani wakazi wa Mtwara watanufaika na gesi hiyo, huku tayari Rais Jakaya Kikwete akiwa ameshazindua ujenzi wa bomba kwenda Dar es Salaam. Wametaka ujenzi huo usitishwe.

Pia wamesema uamuzi wa kupeleka gesi Dar es Salaam unapingana na tamko la Rais Kikwete alilolitoa kwenye ziara yake mkoani hapa mwaka 2009 kwamba ujiandae kuwa ukanda wa viwanda.

Aidha, wanataka vinu vya kuzalishia gesi vijengwe Mtwara kwa kuwa wanayo maeneo ya kutosha ya ujenzi huo tofauti na Dar es Salaam.

“Tunahitaji viwanda vikubwa vijengwe Mtwara ili kuleta ajira kwa wakazi wa Mtwara na mikoa ya jirani, tuna hofu kutokana na ilivyokuwa kwa wakazi wa Songongo (Lindi) kubaki maskini wakati gesi inazalishwa hapo, yasije yakatukuta sisi, hivyo ni lazima tusimamie rasilimali hii ili iweze kuleta maendeleo,” walisema katika azimio lao.

Wamesema pia kwamba Serikali haijaeleza athari zitakazopatikana kutokana na uchimbaji wa gesi katika eneo hilo na namna itakavyoweza kusaidia kuziondoa, huku wakitaka gharama za uunganishaji wa umeme wa nyumbani zisizidi Sh50,000 ili kila mwananchi aone ananufaika na gesi hiyo.

Waandamanaji hao wamesema gharama za mradi huo wa kusafirisha gesi hadi Dar sa Salaam ni kubwa, hivyo wakashauri Serikali ichimbe gesi ya Dar es Salaam katika kisima namba 7 ili kuepuka hasara.

Katika azimio lao la mwisho, wamemwomba Rais Kikwete kumwondoa madarakani Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Joseph Simbakalia kwa madai kwamba amewakashifu kutokana na madai yao ya kupinga gesi kwenda Dar es Salaam.

Ilielezwa kuwa, awali Simbakalia aliombwa kuwa mgeni rasmi katika maandamano hayo, lakini alikataa na badala yake yalipokewa na Mwenyekiti wa Umoja wa Vyama vya Siasa, Hussein Mussa Amiri.

Desemba 21, mwaka huu katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Mtwara (RCC), kilichoketi kwenye Ukumbi wa Boma, Simbakalia alisema hawezi kushiriki katika maandamano hayo. Maandamano hayo yaliratibiwa na vyama vya siasa vya Chadema, NCCR-Mageuzi, Sau, TLP, APPT Maendeleo, ADC, UDP na DP, yakiwa na kaulimbiu ya ‘gesi kwanza vyama baadaye, hapa hakitoki kitu.’
Kutokana na maandamano hayo, Soko Kuu la Mtwara lilifungwa kwa muda kutoa fursa kwa wafanyabiashara hao kushiriki na barabara kadhaa zilifungwa kwa muda.

Mbali ya watu kujitokeza kwa wingi, pia walibeba mabango yenye ujumbe mbalimbali. “Bandari Bagamoyo, Viwanda Bagamoyo, Gesi Bagamoyo, Mtwara wapuuzi?.... Gesi haitoki hata kama hatujasoma.... Gesi kwanza vyama baadaye, hapa hakitoki kitu.... Kusini tumedharauliwa vya kutosha sasa basi.”

Akisoma tamko la vyama hivyo, Katibu wa umoja huo, Seleman Litope alisema kwa muda mrefu Kusini imekuwa ikiondolewa fursa mbalimbali za maendeleo.

Alitoa mfano wa kung’olewa kwa reli, ukosefu wa usimamizi mzuri wa zao la korosho, ukosefu wa miundombinu ya barabara, kuondolewa kwa Mradi wa Maendeleo ya Ukanda wa Mtwara (Mtwara coridor) na hilo la gesi.

Alisema hali hiyo imesababisha mikoa ya Kusini kuwa nyuma kimaendeleo na kwamba umoja wao unalenga kuhakikisha rasilimali yao hiyo haitoki kwenda kokote kabla ya kuwanufaisha.
 
Source: Mwananchi

No comments:

Post a Comment