Friday, June 22, 2012

LULU AKAANGWA NA MAWAKILI WA SERIKALI JUU YA UMRI WAKE


MAWAKILI wa Serikali jana waliwasilisha vielelezo Mahakama kuu kuthibitisha kwamba umri wa msanii wa filamu Elizabert Michael ni zaidi ya miaka 18.Habari zilizolifikia gazeti hili na kuthibitishwa na mawakili wawili; mmoja wa Lulu na mwingine wa Serikali ambao hawakutaka kutajwa, zimeeleza kuwa vielelezo hivyo vimewasilishwa jana mahakamani hapo.

Habari zimeeleza kuwa moja ya vielelezo hivyo vya Jamhuri ni Mkanda wa video aina ya CD, yenye mahohjiano kati ya mshtakiwa huyo na mtangazaji mmoja nchini.

"Vingine ni maelezo ya mshtakiwa huyo aliyoyatoa polisi wakati alipohojiwa kuhusu tuhuma zinazomkabili, maombi ya hati ya kusafiria (Passport) na maombi ya leseni ya udereva, alisema mmoja wa mawakili hao.


Awali vielelezo hivyo walitakiwa kuviwasilishwa juzi, lakini ilishindikana na badala yake vikawasilishwa jana.


Baada ya vielelezo kesi hiyo itasikilizwa Juni 25 mwaka huu. Lulu anakabiliwa na kesi ya mauaji katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akituhumiwa kumuua msanii mwenzake, Marehemu Steven Kanumba aliyefariki dunia nyumbani kwake Sinza, April 7, 2012.


Hata hivyo umri wake umezua utata baada ya mawakili wake wanaomtetea kudai kuwa bado ni mtoto kwa kuwa ana umri wa miaka 17 na si 18 kama hati ya mashtaka inavyoonyesha.


Hivyo mawakili hao walilazimika kuwasilisha maombi mahakamani kuiomba mahakama iruhusu ufanyike uchunguzi wa umri sahihi wa mshtakiwa huyo na ikiridhika kuwa ni mtoto basi kesi yake iendeshwe kwa misingi ya kesi za watoto wanaokinzana na sheria ili kulinda maslahi yake.


Juni 11, 2012 Mahakama Kuu ilikubali yenyewe kufanya uchunguzi huo kwa lengo la kubaini usahihi wa umri wa mshtakiwa huyo na ikaziagiza na kuzipangia tarehe pande zote katika kesi hiyo kuwasilisha mahakamani hapo vielelezo watakavyovitumia katika hoja zao.


Jopo la mawakili wanaomtetea Lulu likiongozwa na Kennedy Fungamtama Juni 13 waliwasilisha mahakamani hati za viapo vya wazazi wake na vielelezo vingine kikiwemo cheti cha kuzaliwa na cha ubatizo vinavyoonesha kuwa bado ni mtoto.


Lakini taarifa zilizopatikana mahakamani hapo zinaeleza kuwa vielelezo vilivyowasilishwa na Jamhuri vinaonesha kuwa mshtakiwa huyo ni mtu mzima kwa kuwa kwa mujibu wa vielezo hivyo ana umri zaidi ya miaka 18.


Viapo vya wazazi wa mshtakiwa huyo vilivyowasilishwa mahakamani hapo na Makamu wa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Peter Kibatala ambaye ni mmoja wa mawakili wanaomtetea Lulu vinaeleza kuwa mshtakiwa huyo ana umri wa miaka 17.


Viapo hivyo ambavyo Gazeti hili limefanikiwa kuviona ni kiapo cha mama yake Lulu Lucresia Augustin Kalugila, mkazi wa Dar eS Salaam na kiapo cha baba mzazi Michael Kimemeta, mkazi wa Moshi.


Viapo vyote vinaeleza kuwa mshtakiwa huyo alizaliwa April 16, 1995 katika kituo cha Afya Muhimbili na kupewa cheti cha kuzaliwa namba B.0318479 cha Julai 23, 2004.


Pia viapo hivyo vinaeleza kuwa baada ya kuzaliwa mshtakiwa, mama yake alimpa jina la Diana Michael Kimemeta, lakini alimpeleka mtoto huyo Moshi mkoani Kilimanjaro kwa ndugu zake, walimpa jina la Elizabeth, jina la bibi yake Elizabeth Shikana.Source: Ujana Tz Blog


TAIFA KATIKA TASWIRA.

Picha na Freddy Maro.

KUTOKA VIWANJA VYA BUNGE MJINI DODOMA LEO

 Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Anne Makinda (kulia) akibadilishana mawazo na Mbunge wa Kuteuliwa Anna Abdallah (kushoto) leo mjini Dodoma katika viwanja vya Bunge.
Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono akibadilishana mawazo na Naibu Waziri wa     TAMISEMI, Aggrey Mwanrijana mjini Dodoma katika viwanja vya Bunge.  Picha na Tiganya Vincent-Dodoma


RAMADHANI SHAULI AONESHWA MKANDA WA UBINGWA WA IBF AFRICA ATAKAOGOMBANIA IDDI PILI

 Bondia  Ramadhani Shauli akiwa ameushika Mkanda wa I.B.F Africa wakati ulipokuwa ukioneshwa mbele ya waandishi wa habari baada ya kuwasili Dar es salaam jana ukitokea USA mkanda huo utakaogombaniwa na Shauli na bondia Sande Kizito kutoka Uganda utafanyika siku ya Iddi pili katika ukumbi wa Diamond Jubilee kushoto ni Makamu wa Rais wa Kamisheni ya Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC) Madaraka Nyerere na Promota wa mpambano huoMkurugenzi wa Kitwe General Traders, Lucas Rutainirwa
Bondia Nassibu Ramadhani kushoto na Ramadhani Shauli wakifungu mkanda wa ubingwa wa IBF Africa utakaogombaniwa na Ramadhani Shauli kushoto na bondia Sande Kizito kutoka Uganda
 
Ramadhani Shauli akiwa na mkanda wa ubingwa wa IBF Africa .
Bondia  Ramadhani Shauli akiwa ameushika Mkanda wa I.B.F Africa wakati ulipokuwa ukioneshwa mbele ya waandishi wa habari baada ya kuwasili Dar es salaam jana ukitokea USA mkanda huo utakaogombaniwa na Shauli na bondia Sande Kizito kutoka Uganda utafanyika siku ya Iddi pili katika ukumbi wa Diamond Jubilee kushoto ni Makamu wa Rais wa Kamisheni ya Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBC) Madaraka Nyerere na Promota wa mpambano huoMkurugenzi wa Kitwe General Traders, Lucas Rutainirwa  .Picha na www.superdboxingcoach.blogspot.com

RAIS KIKWETE ATEMBELEA SHAMBA LA MFANO KIJIJI CHA CHIKOPELO BAHI, MKOANI DODOMA

 Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, akikagua  shamba la nyanya  na mazao mengine ya mboga pamoja na mizabibu katika shamba linalomilikiwa na kampuni ya kilimo ya Tendaji Trade, lililopo kijiji cha Chikopelo,wilaya ya Bahi, Mkoani Dodoma  leo asubuhi. Kushoto ni mmoja wa wamiliki wa Shamba hilo Bwana Alon Hoven, anayeshirikiana na Bwana Dunstan Mrutu (hayupo pichani). Shamba hilo linamwagiliwa kwa kutumia teknolojia ya  matone (Drip irrigation system).
 Mmoja wa Wamiliki wa Shamba la Mboga katika kijiji cha Chikopelo Bwana Alon Hoven, kimwonesha Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete, baadhi ya mazao yanayozalishwa kwa kutumia mbegu bora pamoja na teknolojia ya ya umwagiliaji wa matone wakati Rais alipotembelea shamba hilo katika kijiji cha Chikopelo, wilayani Bahi,mkoani  Dodoma leo asubuhi.Shamba hilo lenye ukubwa wa hekari mia moja linamilikiwa na kampuni ya kilimo ya Tendaji Trade, chini ya Bwana Dunstan Mrutu na Alon Hoven raia wa Israel.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Rais Kikwete alisifu juhudi za wawekezaji hao kwa kutumia mbinu za kisasa za kilimo na kuwaasa wanakijiji wa Chikopelo kujifunza mbinu bora za kilimo hicho cha mboga ili waweze kupata ufanisi na kuboresha maisha yao. Rais Kikwete alitumia fursa hiyo kuwaonya viongozi wa kijiji cha Chikopelo kutoendelea kuuza ardhi yote kwa wawekezaji na badala yake kutunza na kuilinda kwaajili ya kizazi kijacho.


Kutoka Idara ya Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa Ofisi ya Bunge:Ukweli Kuhusu Mishahara Ya Waheshimiwa Wabunge



Wakati Bunge liko kwenye mchakato wa Bajeti ya 2012/13, yameanza kujitokeza maneno na taarifa mbalimbali juu ya kupanda kwa mishahara ya watumishi wa Umma wakiwemo Wabunge. Mathalani, siku ya Jumatano tarehe 20 Juni 2012, gazeti moja linatokalo kila siku lilikuwa na habari yenye kichwa kisemacho “Mishahara ya Wabunge juu”.

Ofisi ya Bunge imeona ni vyema kutoa ufafanuzi juu ya suala zima la mishahara ya Wabunge ili umma uweze kuelimika ipasavyo juu ya taratibu zinazotawala jambo hili kama ifuatavyo:

·         Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, ambayo inajumuisha Fungu Na. 42 lenye Bajeti ya Bunge bado haijasomwa Bungeni, na hivyo haiwezekani leo hii kueleza kuwa kuna nyongeza ya bajeti inayohusu mishahara kwa Wabunge.

·         Si kweli kwamba mishahara ya Wabunge imeongezwa toka kiwango wanacholipwa sasa, kwa kuwa mishahara yao kama ilivyo ya watumishi wote wa umma, hurekebishwa kwa waraka maalum  toka Ofisi ya Rais,  na si Kamisheni au Kamati yoyote ya Bunge.

·         Waraka wa mwisho wa toka Ofisi ya Rais unaotoa Masharti ya Kazi ya Mbunge ulitolewa tarehe 25 Oktoba 2010, na kueleza kuwa Mbunge atalipwa mshahara katika ngazi ya LSS (P) 2, na ni waraka huo unaotumika mpaka sasa. 

·         Mapendekezo ya ongezeko la 32% ya Bajeti ya Ofisi ya Bunge yaliyooneshwa kwenye kitabu cha Bajeti namba 2, cha matumizi ya kawaida yaliyowasilishwa mezani ni ya matumizi mengine ambayo hayana uhusiano na ongezeko la mishahara.


Mwisho, Ofisi ya Bunge wakati wote inathamini sana mchango wa vyombo vya habari katika juhudi za kuelimisha umma juu ya kazi za chombo chao cha uwakilishi. Hata hivyo, Ofisi inasikitishwa sana na habari za upotoshaji zinazotolewa kwa lengo la kujenga chuki kati ya Wabunge na watu wanao wawakilisha.

Kwa mantiki hiyo, tunazidi kuwasihi Waandishi waandike habari au makala baada ya kufanya utafiti wa kina kuhusu jambo husika na pale inapobidi waweze kupata ufafanuzi toka Idara husika katika Ofisi ya Bunge, ili kuepuka kuupotosha umma.


Imetolewa na:
Idara ya Habari, Elimu kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa
Ofisi ya Bunge,
S.L.P 941, DODOMA.
21 Juni 2012

Waziri Mkuu,Mizengo Pinda Akijibu Maswali Bungeni Mjini Dodoma Leo

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akijibu maswali Bungeni Mjini Dodoma Juni 21,2012.Picha na Ofiisi ya Waziri Mkuu

MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA DK GHARIB BILAL AIWAKILISHA TANZANIA KATIKA MKUTANO WA UMOJA WA MATAIFA KUHUSU MAZINGIRA ENDELEVU JIJINI RIO DE JANEIRO



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal ameiwakilisha Tanzania katika mkutanano wa Mazingira Endelevu jijini Rio De Janeiro unaofanyika jijini hapa ikiwa ni miaka 20 baada ya mkutano kama huo kufanyika mwaka 1992. Katika mkutano wa mwaka 1992, ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Rais wa wakati huo Alhaji Ali Hassan Mwinyi.

Mkutano wa mwaka huu unajadili kuhusu maazimio ya mwaka 1992 na namna yalivyotekelezwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa wapatao 182 huku washiriki katika mkutano huu wakikadiriwa kutoka katika nchi 135. Sambamba na hilo mkutano huu unapitisha maamuzi mapya kuhusu kuiweka dunia na mazingira yake katika hali ya usalama ili yaweze kusaidia vizazi vijavyo. Mkutano huu unafanyika ikiwa ni siku chache tangu kufanyika mkutano wa G-20 uliokuwa ukifanyika nchini Mexico na matokeo ya mkutano huo wa G-20 kwa namna moja ama nyingine yameongeza hamasa ya mkutano huu wa Rio +20. Hamasa kubwa kwa mataifa inabaki juu ya kutazama namna uchumi wa kijani utakavyoweza kusaidia kukuza maendeleo ya maisha ya watu duniani huku maendeleo hayo yakiiacha dunia katika hali ya kawaida katika mazingira yake ya asili. Pia hoja ya kuhusu uzalishaji mkubwa wa gesi joto imepata mjadala mkubwa katika mkutano huu. Maeneo mengine ambayo yanajadiliwa ni kuhusu hali ya chakula duniani huku msukumo ukiwa kutoa uhuru kwa nchi kuzalisha chakula ili kutosheleza wananchi wa kila nchi husika.

Ujumbe wa Tanzania unaotolewa na Mheshimiwa Makamu wa Rais Dkt. Mohammed Gharib Bilal unalenga kuonesha namna Tanzania ilivyo na mikakati sadifu katika utunzaji wa mazingira yake sambamba na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo kikubwa yanachangiwa na nchi kubwa zenye viwanda. Ujumbe huu pia unaakisi nafasi ya nchi za Afrika katika kulinda mazingira pamoja na mikakati ya baadaye inayozingatia uzalishaji bila kuathiri mazingira kwa kiasi kikubwa.

 Katika hotuba yake katika mkutano huu, Mheshimiwa Makamu wa Rais anazungumzia umuhimu wa nchi duniani kuzidi kushikamana katika kuhakikisha dunia inabakia kuwa sehemu bora ya kuishi kwa wanadamu wa sasa na wajao. Kufuatia mantiki hii, Mheshimiwa Makamu wa Rais anayakumbusha mataifa yote kuhakikisha yanazingatia maazimio ya mkutano huu wa Rio +20 ili uwe na mafanikio zaidi ya ule wa mwaka 1992.

Waliombatana na Mheshimiwa Makamu wa Rais na ambao wanashiriki mikutano ya kisekta ni pamoja na Mheshimiwa Terezya Huvisa, Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Fatma Fereji, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais SMZ pamoja na Mheshimiwa Mahadhi J. Maalim, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa. Kundi la Wabunge linawakilishwa na Mheshimiwa James Lembeli, Salehe Pamba na Magdalena Sakaya. Mkutano huu ulioanza Juni 20, 2012 unatarajiwa kumalizika Juni 22, 2012.

Imetolewa na:
 Boniphace Makene
        Press Secretary to the Vice President
 June 21, 2012

No comments:

Post a Comment